ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 12, 2011

Padri Salla kusomewa maelezo kortini leo


Na Daniel Mjema,Moshi
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya kumlawiti mtoto wa kiume wa umri wa miaka 16, inayomkabili Padri Stanslaus  Salla (71) wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, leo unatarajia kumsomea mtuhumiwa maelezo ya awali katika kesi yake.

Padri huyo anakabiliwa na mashtaka ya kumlawiti mtoto huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka jana na baadaye kuwa mtumishi wa ndani wa nyumba ya padri huyo, aliyekuwa katika Parokia ya Kilema ya Jimbo Katoliki la Moshi.

Wakili wa Serikali , Abdalah Chavula, ndiye atakayemsomea padri huyo maelezo hayo  ambayo kisheria yanaelezea namna tukio lilivyotokea, idadi ya mashahidi wa upande wa mashtaka na vielelezo vitakavyowasilishwa mahakamani.


Kusomwa kwa maelezo hayo ya awali, kunafuatia hatua ya Jeshi la Polisi, kuiarifu mahakama hivi karibuni kuwa,  tayari upelelezi wa kesi hiyo inayovuta hisia za waumini wa Kanisa Katoliki na wananchi wa Mkoa Kilimanjaro kwa jumla, umekamilia.

Padri huyo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 6 mwaka jana, miezi miwili baada ya kutokea kwa  tukio hilo lililomlazimisha  kutoweka hadi alipojisalimisha mwenyewe katika ofisi ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng'hoboko.

Siku hiyo, wakili Chavulla alidai kortini kuwa usiku wa Oktoba 30 mwaka jana, katika eneo la Kilema Leso, Moshi Vijijini, Padri huyo alimwingilia kinyume cha maumbile kijana wa umri wa miaka 16.

Wakili huyo alidai kuwa kitendo hicho ni kosa chini ya kifungu namba 154 (1) (a) cha sura namba 16 cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2002.Padri huyo alikanusha mashtaka dhidi yake na yuko nje kwa dhamana.


Mwananchi

No comments: