ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 24, 2011

Bastola yamponza Rage Igunga

Mhe. Aden Rage akiwa na bastola kiunoni
Mwandishi wetu
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, amewaagiza polisi kumhoji Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, kuhusu hatua yake ya kupanda jukwaani na bastola kiunoni.  Taarifa iliyopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ambao hawakupenda kutajwa, ilisema polisi wameagizwa kuwa baada ya kumhoji mbunge huyo, wawasilishe ripoti hiyo kwake haraka iwezekanavyo.  


Miongoni mwa mambo ambayo polisi wameelekezwa kumhoji Rage ni pamoja na endapo anaimiliki bastola hiyo kihalali. Mambo mengine ni sababu alizoeleza wakati anaiomba bastola hiyo na hatua yake ya kwenda nayo kwenye mkutano wa hadhara.

“Tunasubiri taarifa, tumewaagiza polisi wamhoji. Tunataka kujua mambo matatu; kama silaha hiyo anaimiliki kihalali, pili madhumuni aliyoiombea na tatu kwenda nayo kwenye public meeting (mkutano wa hadhara) wakati kuna watoto, wanawake na watu wa aina mbalimbali,” kilisema chanzo chetu cha habari kikimnukuu Nahodha na kuongeza:  “Haiwezekani kwenda na silaha tena nje nje kwenye mkutano kama ule. Sasa tunasubiri taarifa ya polisi.”

CUF wawatuhumu CCM
Wakati huo huo Geofrey Nyang’oro anaripoti kutoka Igunga kuwa, CUF kimelitaka Jeshi la Polisi kumkamata na kumchukulia hatua kali, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana ya CCM Taifa (UVCCM), Martine Shigela kutokana na msafara wake kumshambulia kiongozi wa CUF.   Akizungumza na waandishi wa habari Mjini hapa jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (bara), Julius Mtatiro, alisema kitendo cha msafara wa katibu huyo kushambulia mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya CUF ni uchokozi usiokubalika. 

 ”Mwenyekiti wa Jumuiya ya  Wazazi wa chama chetu kutoka katika   kijiji cha  Iyogelo Tarafa ya Igurubi mjini hapa   Salum Masanja (55) amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili kutokana na tukio hilo,”alisema Ntatiro.   Habari zinasema Masanja alipigwa juzi majira ya saa tisa mchana nyumbani kwake katika Kijiji cha Iyogelo Kata ya Kining’inalo alipokuwa akipandisha bendera ya chake.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo, Masanja alisema alipigwa na watu wanne huku mmoja akimtambua baada ya kushuka kwenye gari moja jeupe lililokuwa kwenye msafara wa CCM.  “Zilipita gari tatu nyeupe zikiwa zinapeperusha bendera za CCM, gari moja la nyuma lilisimama na watu wanne wakateremka na kunitaka kushusha benderea hiyo,”alisema Masanja.  

Alisema baada ya kauli hiyo yeye alikataa ndipo walipompiga ngwala na kuanguka chini kisha kuanza kumshambulia kwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili na kumsababisha apoteze fahamu kwa muda wa saa mmoja.   “Zilikuwa gari tatu zilizokuwa katika msafara wa CCM uliokuwa, ukiongozwa na Shigella, zilipofika karibu na mimi gari la nyuma lilisimama na watu hao kunifuata ndipo waliponiamuru nishushe bendera hiyo na kupandisha ya CCM,” alisema Masanja.  

Alisema katika watu waliomshambulia alimtambua mtu mmoja aliyekuwa kiongozi wa msafara ambaye ni Katibu Mkuu wa UVCCM, Shigela. 

Tamko la CUF
Chama cha CUF kimelaani tukio hilo na kulitaka Jeshi la Polisi kumkamata mara moja Shigela na kumchukulia hatua vinginevyo Igunga haitakalika.   Mtatiro alionya kuwa CCM kama wafuasi wa CUF nao watajibu mapigo.  Alisema CUF kwa sasa ni chama kisichopenda kuendekeza vurugu,  lakini akasisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na wafuasi wa CCM ni uchokozi wa wawazi usikubalika.  

“Martine Shigela anafahamika, na kama Polisi watashindwa kuchukua hatua sisi tutachukua hatua wenyewe, tuna uwezo huo na tukianza kuwapiga wafuasi wa CCM tutawashambulia jimbo zima,”alisema Mtatiro.   “Sisi tumekaa kimya muda wote siyo hatuwezi kufanya vurugu, bali tunapambana kuona sheria, kanuni na taratibu zinafuata katika nchi hii, tunaliomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua na kama halitachukua hatua sisi CUF tunafanya kazi hiyo wenyewe,”alisema Mtatiro. 

Mtatiro alisistiza kuwa chama chao hakipo Igunga kwa ajili  ya kufanya vurugu bali kampeni za kistaarabu za kutangaza sera zake na kutaka mbunge wao achaguliwe na wananchi   Majira ya saa 4:00 asubuhi Mtatiro akiwa ameongozana na wajumbe mbalimbali wa CUF akiwamo Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama hicho Mkoa wa Tabora Magdalena Sakaya, walivamia Hodi za Hospitali ya Wilaya na kukuta majeruhi hiyo akiwa hajapatiwa tiba tangu kufikishwa kwake hosipitalini hapo juzi saa 12.00.  

Kamishina Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Telesphory Anacleth, alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa tayari hatua za awali zimechukuliwa.   Alisema mara baada ya kupata taarifa hizo Polisi walifika eneo la tukio juzi na kufanya mahojiano na Masanja pamoja na watu mbalimbali na kwamba jeshi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na tayari limeshafungua kesi ya shambulio la kudhuru mwili.

Mgombea acharuka
Baada ya kupata taarifa za kupigwa kwa kiongozi huyo, mgombea wa CUF, Leopold Mahona alizungumza kwa ukali na kusema atakuwa wa kwanza kuvuruga uchaguzi huo kama hatua hazitachuliwa dhidi ya wahusika. 

Alisema yeye anagombea ubunge ili awatumikie wananchi na watu wanapowashambulia wanataka aje kumtumikia nani katika utumishi wake. 

“Nimesikitishwa na tukio hilo, mimi nagombea ili niwatumikie wananchi  ili waondokane na umasikini unaotukabiri, inapotokea CCM wanakwenda kuwapiga na kuwadhuru wanataka mimi niwatumikie wakinanani, ninachosema CCM waombe radhi kwa hili, la sivyo uchaguzi hautafanyika,”alisema Mahona alipokuwa akihutubia wakazi wa kata ya Nyandekwa.

UV CCM waruka kimanga
Kwa upande wake, Shigela amekanusha tuhuma hizo na kuelezea masikitiko yake kwa watu kupigwa.   “Mimi ninasikitishwa na kitendo cha watu kupigwa Igunga, sisi kama vijana wa CCM tunasikitishwa na tendo hilo na hatuhusiki na watu kupigwa,”alisema Shigela.  Kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake kuwa majeruhi alisema “labda ananifahamu kwa kuniona kwenye TV. 

Shigela alisisitiza kuwa yeye na chama chake hakihusika na kuhusu ushahidi aliotoa akasema lanbada mtu huyo awe amefundishwa.   “Nipo Igunga wiki ya pili sasa mbona sijatuhumiwa kuamuru watu kushusha bendera hiyo kwanini iwe sasa na Iyogelo.?alihoji na kuongeza kuwa chama hicho hakihusika na tuhuma hizo.  

Mkutano wa Bakwata wavunjika
Katika hatua nyingine 'Vazi la hijab' jana lilivunja Mkutano wa Bakwata na waandishi wa habari baada ya baadhi ya viongozi wa Baraza hilo Kuu la Waislamu, kushindwa kueleza maana yake.  Mkutano huo uliitishwa na  Katibu wa Bakwata Wilaya Igunga, Maulid Athman Mussa ambaye alitoa tamko la kukilalamikia Chadema kwamba kiliudhalilisha uislamu katika sakata baina ya cahama hicho na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.

Kuvunjika kwa mkutano huo kulitokana na maswali yaliyoulizwa kwamba vazi la hijabu linalodaiwa kudhalilisha dini hiyo inabidi liweje, hivyo viongozi hao kupandwa na jazba.

Maswali hayo yalionekana kuwachanganya na kuwapandisha jazba viongozi hao, lakini wakijitahidi kutoa ufafanuzi ingawa wao wenyewe walionekana kupishana kauli.  

Shehe wa wilaya, Ally Rage alisema, hijabu inanatakiwa isitiri mwili wote wa mwanamke wa kiislamu na kuacha tu sehemu ya uso wake ndio ionekane.  Ufafanuzi huo ulionekana kushahibiana na wa mwanamke mmoja wa Kiislamu aliyekuwepo ndani ya mkutano huo, Amina Billal aliyekuwa amevaa Hijabu aliyesema ni lazima lifunike miguu na mikono.  

“Hijabu ni vazi la mwanamke wa Kiislamu linalositiri mwili ambalo akivaa nguo yenye mikono mirefu ni lazima liwe refu hadi chini,”alisema Amina na kuwaonyesha wanahabari vazi lake lilikuwa limefunika mikono na miguu.   Kutokana na maelezo hayo, waandishi wa habari waliwataka viongozi hao watazame picha za tukio la Chadema na Kimario katika gazeti moja walilokuwa nalo meza kuu (sio Mwananchi) na waeleze kama DC alivaa hijabu au mtandio. 

Hata hivyo, katika kujibu maswali hayo, kiongozi mmoja alitumia aya za kitabu kitakatifu cha Quaran akisema Hijabu lazima lifunike nywele kwa vile ni haramu mwanamke wa Kiislamu kuonekana nywele zake.   Majibu hayo bado yalionekana kujichanga zaidi na kushindwa kufafanua kama mkuu huyo wa wilaya alikuwa amevaa jijabu au mtandio hali iliyomsukuma Imamu wa msikiti huo, Swalehe Hamisi kufafanua zaidi.  Imamu alisema vazi la hijabu liko katika aina tatu moja likiwa ni lile lililokuwa likivaliwa na wake za mtume Mohamed ambalo lilikuwa likifunika maeneo yote ya mwili bila kuacha sehemu moja ya mwili inayoonekana.  

“Vazi la pili la mwanamke wa Kiislamu ni lile lilokuwa likivaliwa na wafanyakazi kwa maana ya wakulima ambalo lilikuwa likimsitiri mwanamke mwili wote isipokuwa sehemu ya usoni tu,”alisema.  Alifafanua hijabu ya tatu, Imamu huyo alisema ni vazi ambalo linamfanya mwanamke asiwe amejisetiri mwili wote na kwamba vazi hilo linamruhusu mwanamke huyo kusogelewa tu na ndugu wa damu na si mtu mwingine.

 “Hawa Chadema wao walienda kumwondolea hijabu mwanamke wa Kiislamu ambaye hawajazaliwa naye tumbo moja na sio ndugu zake kabisa…hawakupaswa kumsogelea kabisa DC,”alisema Imamu huyo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: