Kipengele cha mwisho wiki iliyopita, nilikutaka usithubutu kuwasiliana na mtu ambaye umeweka lengo la kuachana naye.
Ukweli ni kwamba unapomwalika mtu, kumpigia simu au kumtumia ujumbe ni kama unamtia moyo na kumfanya aamini kuwa unampenda na kumjali.
Kama yeye ndiye anayekutumia ujumbe, unaweza kujibu kwa mkato. Ikiwa mhusika ni mwelewa atakushtukia mapema. Ataona jitihada za mawasiliano anafanya yeye, hivyo atatafakari na kugundua haupo naye tena.
AKIKUITA KATAA!
Iwapo kweli umedhamiria kumaliza uhusiano wako na mwenzako, jaribu kukataa mialiko anayokupa, mathalani kwa ajili ya chakula cha pamoja cha mchana. Pia kama atasema atakufanyia jambo fulani, kataa kiaina.
Fanya vivyo hivyo kwa matukio yote ya kijamii. Kataa mialiko kwa njia ambayo hatakushtukia haraka kuwa humhitaji tena, bali aje kushtuka baadaye atakapojumlisha matukio.
Katika hatua za awali, hii itamaanisha kuwa utakosa kwenye matukio fulani ambayo wewe mwenyewe ungependelea kuyahudhuria, lakini huna la kufanya, maana umeazimia kumaliza uhusiano wako na mpenzi au rafiki yako.
Unapotaka kupeleka ujumbe kwa mpenzi wako kuwa hayupo tena moyoni mwako, lazima tu ujitolee kupata hasara katika baadhi ya mambo. Kumbuka kuwa huhitaji tena uhusiano wako na mwenzako.
PUNGUZA MWITIKIO WAKE
Kuna wakati ambapo rafiki au mpenzi wako akifanya au kusema jambo, utatakiwa kuonesha mwitikio. Kama umeshadhamiria kuachana naye, onesha mwitikio wa shingo upande.
Kama mhusika atabaini jinsi ulivyoitikia kwa shingo upande, utakuwa umepeleka ujumbe maridhawa, kwamba huna tena furaha na uhusiano wenu na kwamba unahisi ni wakati muafaka wa kumaliza mambo.
Kuna mazingira ambayo hutaepuka kumwitikia mpenzi au rafiki unayetaka kumpiga chini. Kwa sababu hiyo, ndiyo maana unapaswa kumwitikia lakini katika hali ambayo inaonesha kana kwamba huna habari naye sana.
Unapomwitikia mpenzi wako kwa shingo upande, unamwonesha kuwa hana tena kipaumbele kwako, jambo ambalo litamfanya yeye mwenyewe kuona kuwa yamkini ni wakati muafaka wa kupunguza moto wake kwako.
PUNGUZA UKARIBU NAYE
Kama umekuwa na mazoea ya kuwa karibu na mpenzi wako kama ilivyo kawaida, anza kujenga mazingira ya kujitenga naye mnapokuwa mbele za watu, ili aweze kuhisi mabadiliko katika mwenendo wako.
Haina maana kuwa usizungumze naye, kaa naye karibu na uzungumze naye kama kawaida, lakini majibu yako yawe ya mkato. Pia usikae karibu naye sana, maana namna hiyo utalazimika kuzungumza naye na kukaribisha lugha yake ya matendo.
Lakini kama itawezekana, jishughulishe zaidi kuzungumza na watu wengine ili kwa kiasi fulani huyo mwenzako aweze kuona kuwa haumpi kipaumbele.
ONESHA WATU KWAMBA HAUPO NAYE
Bila kulazimika kumfedhehesha mwenzako, chukua hatua za kuuonesha umma unaowazunguka kuwa yeye si tena mdau muhimu katika maisha yako, mathalani kwa kutomwalika kwenye shughuli muhimu ambazo ulizoea kumwalika.
Unapolazimika kumwalika, weka mipaka katika mazungumzo yako na yeye. Hata hivyo, haishauriwi kuwatangazia marafiki zako wengine kuwa unataka kumtenga mpenzi au rafiki yako huyo, maana namna hiyo watajiwa na fikra kuwa yamkini ana matatizo kumbe kwa hakika kama kuna mwenye matatizo basi ni wewe (au unavyopaswa kuwafanya watu waamini).
Kama unataka kuwa mstaarabu, hakikisha kuwa hakuna mtu mwingine anayeingia katika mchakato huu wa kumbwaga mpenzi au rafiki yako, kwani hili ni suala lako binafsi.
USIJIBEBESHE MZIGO
Hakuna haja ya kubeba mzigo wa uhusiano ambao huna maslahi nao. Japo baadhi ya wanawake huwalalamikia wanaume ambao huwachezea kisha wakawaacha, ukweli ni kwamba hupaswi kuendelea na uhusiano ambao haukupi kile ukitakacho.
Watu wengi walishafanya hivi na kufanikiwa kumaliza vema uhusiano wao na wapenzi wao. Hakuna ubaya wowote kufanya hivi pale unapoona kuwa mwenzako anakupeleka kule ambako usingependa kwenda kwa sasa.
Iwapo utatokea mgogoro wowote, au mpenzi wako akawa na malalamiko, bahati nzuri tayari unazo sababu zako ambazo umetakiwa kuziweka bayana mawazoni.
Hapo ndipo utakapozianika mbele yake na kumweleza msimamo wako mpya. Hata hivyo, utaratibu huu wa kumaliza uhusiano unafaa zaidi kwa wapenzi ambao uhusiano wao haujajenga mizizi, au wale ambao ni marafiki wa kawaida.
Kama uhusiano wako na mwenzako umeshaota mizizi, zipo tahadhari nyingi zaidi za kuchukua, maana ulishampotezea mwenzio muda mwingi.
Global Publishers
1 comment:
Kwa mara ya kwanza nimeingia humu na nimekutana na kitu nnachokihitaji. Kuna mtu ananisumbua sana, alivyonitongoza alinambia kagombana na girlfriend wake, mwaka karibia na miezi mitatu sasa mwanamke yupo tena anaishi nae nyumba moja, kila siku ananipa hadithi. Nimechoka, na mimi nahitaji wangu, taratibu nafuata maelekezo hapa na nammwaga kapata alichotaka, its time i move on. Asante
Post a Comment