ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 23, 2011

Shellukindo ahojiwa kamati ya Jairo


Beatrice Shellukindo, ambao watahojiwa kuhusiana na tuhuma za kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge, zinazomkabili Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kufikia jana walikuwa wamekwisha kuhojiwa na Kamati Teule ya Bunge inayochunguza tuhuma hizo.
Mbali na kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge, Luhanjo anakabiliwa pia na tuhuma ya kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo, kupisha uchunguzi dhidi yake kwa tuhuma za kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/12.
Habari za kuhojiwa kwa Shellukindo, zilipatikana juzi zikiwa zimepita siku tisa tangu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ramo Makani, kukaririwa na NIPASHE akisema kuwa kamati yake ilikuwa imekwisha kuwahoji watu zaidi ya 10 kuhusiana na tuhuma hizo.

Shellukindo ndiye ‘aliyeibua tuhuma dhidi ya Jairo katika Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi uliomalizika Agosti 26, mwaka huu.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo, zinaeleza kuwa Shellukindo alihojiwa hivi karibuni, zikiwa zimesalia siku chache kabla ya vigogo wengine wanaoguswa na tuhuma zinazomkabili Luhanjo, kuhojiwa.
Makani, ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), alipoulizwa na NIPASHE jana alithibitisha kuhojiwa nusu ya watu wanaoguswa na tuhuma hizo.
Kuhusiana na kuhojiwa Shellukindo, alisema taratibu za kazi za kamati yake zinamzuia kumtaja mtu aliyekwisha kuhojiwa au anayetaka kuhojiwa.
“Tunaendelea vizuri na hadi sasa zaidi ya asilimia 50 ya watu wamekwishahojiwa. Kulingana na taratibu za kazi ya kamati, nisingependa kumtaja niliyemhoji na nitakayemhoji kesho,” alisema Makani.
Shellukindo mwenyewe alipotafutwa jana kuthibitisha habari hizo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Hata hivyo, habari zinasema kuwa Shellukindo alipohojiwa na kamati hiyo alisema kuwa aliibua tuhuma hizo kwa maslahi ya taifa na wala hakuwa na hila za kumkandamiza mtu yeyote.
Makani alisema idadi ya watu wanaohojiwa ni kubwa na kwamba, kufikia jana walikuwa bado hawajawafikia vigogo wanaoguswa na tuhuma zinazomkabili Luhanjo.
Septemba 15, Makani alikaririwa na NIPASHE akisema mahojiano yanayofanywa na kamati yake, yatakamilika ndani ya wiki mbili, kuanzia siku hiyo na kwamba, ndani ya kipindi hicho wanatarajiwa vigogo wote wa serikali wanaoguswa na tuhuma zinazomkabili Jairo, akiwamo Luhanjo watakuwa wamehojiwa.
Katika tuhuma hizo, Luhanjo anadaiwa kutamka mbele ya waandishi wa habari kwamba: “Alichofanya Jairo ni utaratibu wa kawaida kabisa ...na kama Jairo ataweza kuwashtaki waliomdhalilisha ni yeye tu.”
Vigogo wengine watakaohojiwa na kamati hiyo, ni Jairo, Waziri wa Wizara hiyo, William Ngeleja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.
Awali, Makani aliliambia NIPASHE kuwa kati ya watakaohojiwa, baadhi wanatoka mikoani, lakini walio wengi wanatoka jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo yenye wajumbe watano, ilitangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, muda mfupi kabla ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi, Agosti 26, mwaka huu.
Iliundwa baada ya wabunge kuridhia ufanyika uchunguzi huo.
Miongoni mwa kazi zake, ni pamoja na kuchunguza sakata lote la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Mbali na Makani, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo, ni Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).
Kamati hiyo inafanya kazi kwa kuongozwa na hadidu za rejea tano; ya kwanza ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya wizara bungeni.
Hadidu rejea hiyo ya kwanza itakuwa na vipengele vitatu; ambavyo ni kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.
Hadidu rejea ya pili, ni kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Jairo kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Pia kuchunguza mfumo wa serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kualiarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.
Hadidu rejea ya nne, ni kuchunguzwa kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Luhanjo, kwa suala la Jairo na kubaini iwapo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.
Ya tano, ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na masuala hayo.
Kamati hiyo ilipewa muda wa kufanya kazi huyo usiozidi wiki nane (miezi miwili) na kuwasilisha taarifa yake wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge, utakaoanza Novemba 8, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: