ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 25, 2011

Wachungaji wanne mbaroni wakidaiwa kuteketeza Koran


Sheilla Sezzy,Mwanza
 POLISI  mkoani  Mwanza, wanawashikilia wachungaji wanne wa Kanisa la Tanzania Assemblise of God, kwa tuhuma za kuiteketeza  kwa moto Koran Tukufu kwa madai kuwa ni ushetani.Polisi pia wamefungua majalada matatu yanayohusu  vurugu  zilizosababisha kuteketezwa kwa kanisa na  msikiti,  jijini Mwanza.

Hayo yalisemwa jana na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow ,katika  taarifa  yake kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa.Kikao kilichopokea taarifa hiyo inayohusu vurugu za kidini zilizotokea juzi katika Mtaa wa Lumala, jijini Mwanza, kiliwahusisha pia viongozi wa madhehebu  ya Kiislamu  na  ya Kikristo.




Barlow alisema uchunguzi wa awali wa tukio hilo umethibitisha kuteketezwa kwa moto, Koran Tukufu.Akifafanua kuhusu tukio hilo, Barlow alisema lilijitokeza baada ya wachungaji hao kwenda  katika nyumba ya Husina Hamisi, kwa ajili ya kumuombea baada ya kumfanyia maombi ya kuokoka.

Alisema baadaye, wachungaji hao, kuchoma moto Koran, iliyokuwa ikitumiwa mama huyo.Alisema  katika mahojiano naye, Husina alikiri kuwa kitabu kilichochomwa moto  na wachungaji hao ni Koran Tukufu na kwamba kauli hiyo iliiungwa mkono na  mtoto wa Husina mwenye umri wa miaka 10.

Alisema taarifa za kitendo hicho, zilienea miongoni mwa waumini mwa Kiislamu ambao baadaye walikwenda katika Mtaa wa Lumala na kuchoma moto kanisa.Barlow alisemahata hivyo polisi  kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuuzima moto huo ambao haukuleta  athari zozote  kwa binadamu.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, Waislamu pia walitishia  kuendelea kuyachoma moto  makanisa mengine, hatua iliyowalazimisha polisi  kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali.


Alisema baadaye polisi walibaini kopo lililokuwa na  petrol, likiwa limetupwa  ndani ya Msikiti wa Ibungiro, ulioko Nyamanoro.Alisema kopo hilo lilitupwa na watu waliokuwa na lengo la kutaka kuchoma msikiti huo.Kamanda huyo alisema kufuatia tukio, polisi wanaendelea  na upelelezi huku wakiendelea kuimarisha ulinzi mkali.

Kwa mujibu wa ofisa huyo wa polisi,  wachungaji hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka wakati polisi wakiendelea kuwasaka waliohusika  katika  majaribio ya kuchoma moto  msikiti na waliochoma kanisa.
 Mwananchi

No comments: