Watanzania waishio Marekani wamesifia jitihada za Rais Kikwete za kuwashirikisha katika maendeleo ya Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi.
Hayo yalisemwa jana kwenye kilele cha Kongamano la Tatu la Watanzania Waishio Ughaibuni mjini hapa ambapo Watanzania zaidi ya 500 wamehudhuria pamoja na makampuni, mashirika ya umma na binafsi zaidi ya 15 kutoka Tanzania yamehudhuria kongamano hilo
. Miongoni mwa mambo yaliyowavutia ni hotuba ya Rais Kikwete ambayo alifafanua masuala ya uraia pacha na haki ya kupiga kura kwa Watanzania walioko nje ya nchi kuingizwa kwenye mjadala wa Katiba mpya.
Rais Kikwete aliwasihi Watanzania wasirudi nyuma katika kujiletea maendeleo hata kama wako mbali na nyumbani.
Rais wa DICOTA Dk. Ndaga Mwakabuta ,alisema: “Tumeguswa na ujio wa Rais Kikwete na Mawaziri walioongozana naye na Makatibu Wakuu hapa Marekani.
Tumeona jinsi Rais anavyojali mchango wetu, ana imani na sisi, ametushirikisha na kuelekeza wasaidizi wake na watendaji waungane na sisi kwenye suala zima la uraia wa nchi mbili, hii ni faraja kubwa kwetu.”
Wengine walisema Kongamano hili limewabadilisha fikra zao kuhusu utendaji kazi wa Serikali, ambapo sasa wana imani ya kupata mafanikio kutokana na jitihada zinazofanywa na serikali ili kuwasaidia kupeleka maendeleo yao nyumbani na hatimaye kuinua uchumi wa nchi.
Kongamano la DICOTA (Baraza la Watanzania Waishio Ughaibuni Marekani) hufanyika kila mwaka kuanzia mwaka 2009 kwa kuwaleta pamoja Watanzania kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
OOH please give me a breaaak!
Post a Comment