ANGALIA LIVE NEWS
Monday, September 26, 2011
Wiki ya kufa, kupona Igunga
HESABU ZAVIBAKISHA CUF, CHADEMA NA CCM KATIKA KINYANG’ANYORO
Daniel Mjema, Igunga
KAMPENI za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga, leo zinaingia katika wiki ya lala salama huku tathmini ikionyesha kuwa mchuano mkali ni baina ya vyama vitatu, licha ya vyama nane kusimamisha wagombea wake.
Vyama vyenye ushawishi mkubwa kisiasa jimboni humo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, ni CCM kilichomsimamisha Dk Dalaly Kafumu, CUF kilichomsimamisha Leopard Mahona na Chadema ambacho kimemsimaisha, Joseph Kashindye.
Uchaguzi huo pia unavishirikisha vyama vya SAU, UPDP, DP, AFP na Chausta, lakini baadhi yake kampeni zake zinaendeshwa kwa kusuasua, huku vingine vikishindwa kabisa kufanya kampeni hizo.
Katika muda wa wiki mbili za kampeni Igunga, kumekuwa na matukio baadhi ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kutuhumiana kwa matukio ya uhalifu, ukiwamokampeni chafu, ubakaji, kumwagiwa tindikali, udhalilishaji na hata vitisho vya kutumia silaha za moto kama bastola.
Mvutano mkali zaidi upo baina ya CCM na Chadema, ambavyo makada wake wamekuwa wakipiga kambi za muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kulala katika maeneo yenye idadi kubwa ya wapigakura.
Juzi Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi alitua kukiongezea nguvu chama chake, lakini tayari CCM kilikwishaongeza wapiga kampeni wake wakiwamo, Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho Philip Mangula. Kwa upande wake CUF kinajivunia mtaji wa kura 11,000 ilizopata katika uchaguzi wa mwaka jana.
Mbinu nyingine ambayo imekuwa ikitumiwa katika kampeni hizo ni wagombea kujinadi kwa lugha ya kisukuma kutokana na wapigakura wengi wa jimbo hilo kuzungumza lugha hiyo ikilinganishwa na Kiswahili.
Hali hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu wanahabari kufuatilia mikutano hiyo kutokana na wengi kutofahamu lugha hiyo, isipokuwa pale anapokuwapo mkalimani wa kutafsiri maneno husika Kiswahili.
Katika wiki ya mwisho iyaoanza leo, viongozi wa kitaifa wa vyama vyenye ushindani, wanatarajiwa kuhamia Igunga, ili kunadi sera za wagombea wao ili kujihakikikisha ushindi.
Inachojivunia CCM
CCM ambacho kinadai kuwa na mtaji wa kura 39,000 ilizozipata katika uchaguzi mkuu uliomalizika Oktoba mwaka jana, kimekuwa kikijivunia mfumo wa uongozi kuanzia ngazi ya mabalozi, shina, kata hadi wilaya.
Chama hicho kinaamini kuwa kama viongozi wao hao hawatakisaliti basi kina uhakika wa kutetea kiti hicho kilichoachwa wazi na Rostam Aziz aliyejiuzulu huku kikiamini kushinda kwa zaidi ya asilimia 60.
Mbali na uongozi huo, lakini chama hicho kina madiwani 24 kati ya 26 na kinaamini kuwa madiwani hao pia wana ushawishi mkubwa kwa vile walichaguliwa na wananchi kwa kura.
Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama wiki iliyopita alisema chama chake pia kinajivunia sera nzuri kwenye huduma za jamii ikiwamo mradi mkubwa wa maji wa Shinyanga-Nzega-Igunga ambao utafanya tatizo sugu la maji Igunga kuwa historia.
CCM kimejenga imani kwamba tuhuma dhidi ya Chadema kwamba wanafanya vurugu, zinaweza kukisadia kuendelea kuliongoza jimbo hilo ambalo halijapata kuwa na mwakilishi wa upinzani.
Baadhi ya makada wa CCM wanaweka wazi kwamba Chadema ambacho ni chama kikii cha upinzani nchini, kimejikuta kikisigana na CUF ambao pia ni wapinzani na kwamba CCM wanaweza kunufaishwa na hali hiyo.
Kwa mtizamo huo, CCM kinaamini CUF kitasaidia kupunguza kura za Chadema ambacho hakina mizizi jimboni humo ikilinganisha na CUF ambacho kilishiriki uchaguzi mkuu 2010 na kunyakua kura 11,000.
Hivyo ipo imani kwamba Chadema na CUF vinaweza kujikuta vikigawana kura za wale wanaounga mkono upinzani, hivyo CCM kushinda kwa urahisi.
Vijana kuwabeba Chadema
Kwa upande wake Chadema ambacho ni chama kipya katika siasa za Igunga, kinaamini kitashinda uchaguzi huo kwa kile kinachodai ni kufanikiwa kujipenyeza katika kundi la vijana ambao ni wengi.
Hakuna ubishi kwamba katika mikutano ya chama hicho, kundi kubwa linaloonekana kukiunga mkono ni vijana ambao wanaamini matatizo makubwa ya ajira na maisha magumu yamesababishwa na CCM.
Jambo jingine, Chadema kinaamini mgawanyiko ndani ya CCM uliosababishwa na kujiuzulu kwa Rostam, pia utapunguza kura za chama tawala na kuwanufaisha wapinzani.
Wafuasi wa Rostam wanadaiwa ‘kununa’ na kufanya kampeni za chinichini ili kuhakikisha CCM hakishindi uchaguzi huo.
Jambo lingine ambalo Chadema kinaamini litapunguza kura za CCM ni hatua ya kumsimamisha Dk Kafumu katika wakati ambao kuna kelele nyingi kuhusu ufisadi katika sekta ya madini ambayo yanadaiwa kutowanufaisha Watanzania.
Kabla ya kuteuliwa kwake kupeperusha bendera ya CCM, Dk Kafumu alikuwa kamishina wa madini na Chadema na CUF vinatumia hilo kama silaha ya kummaliza mgombea huyo kwamba alishiriki ufisadi.
CUF na mtaji wa kura 11,000
CUF kwa upande wao wanaamini kuwa kura 11,000 kilizozipata 2010, mgawanyiko ndani ya CCM unaotokana na kundi la Rostam na vurugu zinazotokea jimboni humo zitasaidia kukivusha na kushinda.
Mbali na hayo lakini CUF kinaamini kuwa ndicho pekee kimeendesha kampeni za kistaarabu kulinganisha na vyama vingine na kutokana na hulka ya wenyeji kutoshabikia vurugu basi watakipa kura.
Pia CUF kinaamini kwamba mchuano mkali kati ya Chadema na CCM kutavifanya vyama hivyo viwili kugawana kura hivyo wao kupata ushindi kutokana na ushawishi walioufanya kwenye kampeni.
CUF kinaamini mgombea wake ndiye mwenye nguvu na anayekubalika zaidi na kwamba hata 2010 angeweza kuibuka mshindi lakini kutokana na ‘nguvu’ kubwa aliyoitumia Rostam ndio iliyochangia kumwangusha.
Kinachotarajiwa
Kutokana na hali ilivyo na ushindani mkubwa baina ya vyama vya Chadema, CUF na CCM, wadadisi wa siasa wanasema lolote linaweza kutokea katika jimbo hilo.
Wiki ya mwisho ya kampeni hizi inaweza kutoa mwelekeo wa nani atakuwa mshindi lakini kwa mtizamo wa kidadisi, hadi sasa hakuna chama chochote chenye uhakika wa ushindi.
Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika Oktoba 2 huku wapiga kura waliojiandikisha wakiwa 170,000 lakini wanaweza wasijitokeze wote kama ilivyotokea mwaka jana ambapo ni asilimia 40 waliojitokeza.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment