Polisi wakichukua mwili wa marehemu baada ya kufariki kwa kuungua kwa moto alipokua amefungiwa kwa deni la 50,000/=
Mkazi wa Jiji la Mbeya, Hansen Mtono (30), amekufa kwa kuungua kwa moto katika chumba alichofungiwa ndani ya baa moja, kwa kile kinachodaiwa kuwa alishindwa kulipa Sh. 50,000 ambazo alikuwa akidaiwa baada ya kunywa pombe.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 11:30 jioni, katika baa ya Omega, iliyopo katika kitongoji cha Isanga, mjini hapa, ikiwa ni siku ya pili tangu mkazi huyo afungiwe ndani ya chumba cha baa hiyo. Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia NIPASHE kuwa, Septemba 28 mwaka huu, Hansen, mkazi wa eneo la Isanga, alikwenda katika baa hiyo ambako alikunywa pombe na kushindwa kulipa na wakati alipotaka kuondoka majira ya jioni ndipo alikamatwa na wahudumu na kufungiwa katika moja ya chumba cha baa hiyo.
Shuhuda mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Hansen aliendelea kusota ndani ya chumba hicho bila kupewa chakula hadi kesho yake majira ya jioni, ambapo chumba alichokuwemo kijana huyo kilipoonekana kikiwaka moto huku Hansen akipiga kelele za kuomba msaada.
“Tulisikia kelele za Hansen akiomba msaada kupitia katika dirisha la chumba hicho ambalo lilikuwa wazi, lakini kwa kuwa limetengenezwa kwa nondo alishindwa kutoka hadi alipoungua na kufa kutokana na moto huo,” alisema shuhuda huyo.
Alisema baadhi ya watu waliokuwa jirani na eneo hilo walijaribu kuzima moto huo kwa kutumia maji, lakini walishindwa kutokana na moto huo kuwa mkubwa na kuteketeza kabisa chumba alichokuwemo kijana huyo.
Hata hivyo, wakati moto huo ukiendelea kushika kasi, liliwasili gari la Zimamoto la Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambalo lilifanikiwa kuuzima kabla haujaenea katika sehemu nyingine za baa hiyo.
Shuhuda huyo alisema wakati kijana huyo akiendelea kushikiliwa, waliomshikilia waliwasiliana na wazazi wake kwa njia ya simu na kuwataka wapeleke pesa ili wamwachie.
“Inadaiwa kuwa hata mchana leo (jana) waliwapigia simu wazazi wake na kuwataka walete pesa, lakini wazazi wake wakawajibu kuwa kama mtoto wao amekunywa pombe bila kulipa ni vema wakampeleka polisi,” alisema shuhuda huyo.
Bado chanzo cha moto huo hakijajulikana.
Gazeti hili lilifika katika eneo la tukio na kukuta jitihada za kuuzima moto zikiendelea na kushuhudia mwili wa marehemu ukiwa umeharibika vibaya, ukiwa katika kiti aina ya Sofa huku mguu mmoja ukiwa umejikunja.
Baadaye waliwasili Polisi ambao waliuchukua mwili huo na kuondoka nao, huku pia wakimkamata mmiliki wa baa hiyo, Mama Omega au mama Ngwada, pamoja na mhudumu mmoja wa baa hiyo ambaye hakutambulika jina lake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watu wawili wanashikiliwa na Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
Kamanda Nyombi aliwataja wanaoshikiliwa na Polisi kuwa ni Emma Ngwanda (36), mkazi wa eneo la RRM jijini Mbeya na Neria Meshack (20), mkazi wa Isanga.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment