ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 5, 2011

JWTZ yanasa maharamia saba

Raymond Kaminyoge na Patricia Kimelemeta
JESHI la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewakamata maharamia saba waliotaka kuteka meli iliyokuwa ikifanya utafiti wa mafuta Pwani ya Bahari ya Hindi karibu na eneo la Mafia.Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe, alisema hivi sasa jeshi hilo linawashikilia maharamia hao kwa mahojiano zaidi.

Kanali Mgawe alisema kikosi cha wanajeshi hao kilikuwa kwenye doria ya kawaida na kubaini kuwapo kwa tukio hilo la utekaji meli, jambo ambalo liliwafanya kupambana nao na kufanikiwa kuwakamata.

 “Ni kweli tumefanikiwa kuwakamata maharamia saba, ambao walitaka kuteka meli iliyokuwa inafanya utafiti wa mafuta katika bahari yetu, tunawashikilia kwa mahojiano zaidi,” alisema Kanali Mgawe.


Aliongeza kuwa hadi sasa hawajajua makundi ya ugaidi wanakotoka maharamia hao, lakini wanaendelea kuwasaka wengine.Taarifa ya awali iliyotolewa na Msajili wa Meli, E. Wapalila, alisema meli hiyo iliyotaka kutekwa baharini inaitwa Ocean Rig Poseidon.

Taarifa ya Wapalila, ilieleza kuwa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji Majini (MRCC) kinachoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri wa Nchi Kavuna Majini (Sumatra), kilipokea taarifa za tukio hilo Oktoba 3, mwaka huu saa 2:15 usiku.

Ilisema tukio hilo lilitokea umbali wa maili 23 Kusini Mashariki mwa Kisiwa cha Mafia, sawa na maili 82 kutoka Dar es Salaam.Taarifa hizo zilisema maharamia hao walikuwa katika boti ndogo na walishambulia meli hiyo kwa silaha, lakini jaribio hilo lilijibiwa na wanajeshi wa JWTZ na kuwadhibiti.
Mwananchi

No comments: