ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, October 12, 2011
Maria Nyerere: Viongozi wengi hawana maadili
Elias Msuya, Butiama
MKE wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere amesema viongozi wengi wa taifa wamekosa maadili kutokana na kukosa malezi stahili na kuonya kwamba tatizo hilo linaweza kuivuruga nchi kama ilivyotokea katika nchi za Kiarabu zenye utajiri wa mafuta.
Akizungumza jana mara baada ya kumkaribisha nyumbani kwake, Mwitongo Butiama, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara, Mama Nyerere alisema tatizo la ukosefu wa maadili linaanzia katika familia.
Waziri huyo yupo katika Maonyesho ya miaka 50 ya Uhuru yanayofanyika kijijini Butiama alikozaliwa Mwalimu Nyerere. Maonyesho hayo yalifunguliwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi, Oktoba 7 mwaka huu.
Kauli ya Mama Nyerere inakuja kipindi ambacho taifa linatikiswa na ukosefu wa maadili kwa viongozi wa kada mbalimbali wakiwamo wa umma, hali ambayo inaelezwa kuwa kichocheo cha vitendo vya ufisadi katika ofisi mbalimbali za umma tofauti na wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza.
Mama Nyerere alisema maadili yanatokana na malezi katika familia, hivyo wazazi wanapaswa kuzitunza familia zao kikamilifu.
Kutokana na ukubwa wa tatizo alisema: “Ifike mahali tuwe na mafundisho ya jando, ili kuwajenga kimaadili. Shida ya nyumbani itatuliwe kifamilia, lakini tujue tatizo la viongozi wa sasa ni kutokuwa na shule za viongozi.”
Malalamiko ya vijana
Mama Maria pia alisema kumekuwa na wimbi la vijana wengi kuilalamikia Serikali, akisema hiyo ni dalili ya viongozi wa Serikali kutotimiza wajibu wao kwa taifa.
“Kwa kuwa hatukutimiza wajibu wetu kwa taifa, vijana wamekuwa wakinung’unika. Utakuta kijana analaumu chama hadi anataja majina ya viongozi. Walimu wananung’unika, wanafunzi wananung’unika, wakija kwenu na ninyi mnanung’unika, hilo litakuwa taifa gani?”
Alisema msingi wa viongozi bora ni malezi bora katika familia na kwamba viongozi wengi waliopo sasa wana upungufu kutokana na malezi mabovu.
“Kiongozi anatoka katika familia, lakini wengi wana upungufu. Unamwona kiongozi anatembea lakini amejaa upungufu.”
Alikumbusha kuwa hata wakati wa Mwalimu Nyerere, viongozi walikuwa na matatizo, lakini waliyatatua kwa kujadiliana.
Huku akitoa mfano wa vita inayoendelea Libya, Mama Nyerere alionya kwamba nchi inaweza kuingia kwenye matatizo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ikiwa maadili hayatalindwa.
“Tusipolinda maadili, matatizo ya nchi zenye mafuta kama ndugu zetu Waarabu kule Libya yatakuja kwetu,” alisema.
Kuhusu nafasi yake akiwa mke wa Mwalimu Nyerere, alisema haoni kitu kikubwa kwake zaidi ya kuwatumikia wananchi... “Mimi kuwa Mama wa Taifa na mwenzangu Baba wa Taifa ni vitu vidogo sana. Cha msingi ni kutekeleza kazi hizi na zile. Je, huyu ambaye hana chakula wala halindwi au hapati chakula, naye atafanyaje?”
Alizungumzia pia maadili katika vyombo vya habari akisema nako pia kunahitajika uimarishwaji mkubwa wa maadili hayo.
“Kuna waandishi walikuja hapa kunihoji, nikajiuliza hivi hawa wamepita shule ya uandishi wa habari kule Nyegezi St. Augustine? Nilijiuliza moyoni lakini, sikuwaambia. Maana waandishi wanaweza kutumia uandishi wao kama ukali wa upanga. Wanatakiwa nao kuwa na maadili,” alisema.
Kuhusu lishe kwa watoto, Mama Maria alisema: “Ninachosisitiza katika familia ni lishe, shibe na elimu. Mtu akishashiba anasoma kisha anatafuta ajira. Msipowapatia ajira vijana mtawatumia wapi?”
Alikwenda mbali na kusema jamii ya sasa inahitaji kuwa na mafundisho ya jando ili kuijenga kimaadili.
Naibu Waziri
Kwa upande wake, Dk Mukangara aliahidi kuufanyia kazi ushauri wa Mama Nyerere:
“Tunashukuru sana bibi, umezungumzia maadili katika familia na viongozi na maadili ya habari. Hayo yote tutashughulikia kikamilifu. Hata haya ya habari mnajua tena waandishi wetu, tutayashughulikia.”
Awali, mtoto wa Mwalimu Nyerere, Makongoro alikanusha taarifa kwamba familia ya Nyerere imesusia maadhimisho hayo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment