ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 1, 2011

Mvua yaezua mapaa ya nyumba 104 Dar


Moja ya Nyumba iliyoezuliwa paa baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha Mbagala kwa Mangaya,Temeke,Dar es salaam
Fredy Azzah
NYUMBA 104, zimeezuliwa katika Kata ya Mbagala, Dar es Salaam kutokana na kimbunga kilichoambatana na mvua kubwa zilizonyesha katika jana.  Mvua hizo zilizoanza majira ya saa nne asubuhi, zilikuwa zikiongezeka kadri muda ulivyosonga na kufuatiwa na upepo mkali.  Diwani wa Kata ya Mbagala, Agrrey Kayombo alisema zaidi ya nyumba 29, zimeezuliwa kabisa na wakazi wake hawana mahali pa kuishi.

 “Nyumba zote zilizoharibiwa ni 104, kati ya hizo, 29 zimeezuliwa kabisa na hizi ni takwimu ambazo tunazo katika hatua hizi za mwanzo, taarifa zaidi zinaendelea kukusanywa na watendaji kwa hiyo mpaka kesho naweza kuwa na taarifa kamili,” alisema Kayombo.  Alisema taarifa ambazo mpaka sasa hazijapatikana ni pamoja na idadi kamili ya watu walioathiriwa na kimbuga hicho na hasara kamili iliyotokea. 

 Alisema sababu kubwa iliyofanya nyumba hizo kuezuliwa ni upepo mkali ulioambatana na mvua zilizoanza kunyesha katika eneo hilo majira ya saa nne asubuhi jana.  Diwani huyo alieleza kuwa watu watano waliumia katika tukio hilo akiwamo mmoja aliyedondokewa na bati la nyumba. Wote walipelekwa hospitali.  “Watu wanne wamesharudi nyumbani na mmoja bado yupo hospitali, kati ya hawa watu walioumia, mmoja alikuwa ni mama mjamzito ambaye alipigwa na bati,” alisema diwani huyo.

 “Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Mbagala kwa Mangaya na Serenge, vitongoji ambavyo vipo ndani ya Mtaa wa Mangaya,” alisema.  Alisema watu waliopoteza makazi yao jana  walikubaliana kuwa walale kwa majirani wakati uongozi wa wilaya ukiangalia namna ya kushughulikia tatizo hilo.

Alisema viongozi wa Wilaya ya Temeke  watakutana leo kwa ajili ya kuangalia ni kwa namna gani watakavyosaidia watu walioathiriwa na kimbunga hicho.  “Lakini pia tumekubaliana kuwa, jeshi la polisi kwa kushirikiana na ulinzi shirikishi leo watakuwa katika eneo hilo wakihakikisha usalama wa watu na mali zao unakuwapo,” alisema Kayombo.  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa taarifa alizonazo ni nyumba 29 ambazo zimeezuliwa kabisa.

“Kuna nyumba 29 zilizoondolewa paa kabisa na nyumba nyingine zimeezuliwa maeneo mbalimbali lakini bado tathmini inaendelea,” alisema.  Alisema katika tukio hilo, Yusuf Bakari (75), alidondokewa na ukuta na kuumia sehemu mbalimbali za mwili pamoja na kuvunjika mguu. Alisema pia mkewe, Zainab Bakari (60) na kijana wao Hamis Yusuf (30), waliumia.

“Mkewe na Hamis walipelekwa hospitali lakini wameruhusiwa na huyo mzee amelezwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Kamanda Misime.  


Mwananchi

No comments: