ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 11, 2011

Stars yarejea leo, wadau `wafunguka`



Wadau mbalimbali wa soka nchini wamesema kuwa ili Tanzania ifuzu katika fainali za mashindano makubwa ya ndani na nje ya bara la Afrika, ni lazima uandaliwe mkakati wa kuandaa wachezaji vijana ambao watakuwa wamepata misingi bora huku wengine wakisema kuwa tatizo ni kocha wa timu hiyo, Jan Poulsen, wakidai kuwa ameshindwa kuwapa wachezaji wake mbinu sahihi za ushindani.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, juzi ilishindwa kukata tiketi ya kushiriki fainali za mwakani za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kumaliza ikiwa mkiani kwenye msimamo wa Kundi D lililokuwa na nchi za Algeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati na vinara Morocco ambao walifuzu kwa fainali hizo.

Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu, alisema kuwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) lisikwepe lawama na mzigo ni wao ambao wamesababisha Tanzania kuendelea kuwa watazamaji kwenye mashindano hayo makubwa ya soka barani.
Zungu alimtupia lawama pia Poulsen kwa kudai kuwa uwezo wake wa kufundisha ni mdogo na amekuwa akitumia wachezaji wanaocheza nje ambao kiufundi hawafahamu na ameshindwa kushirikiana na Idara ya Ufundi kuzunguka kuangalia vipaji kwenye timu nyingine zinazoshiriki ligi ya Bara na mashindano ya vijana.
"Inasikitisha sana, kama kuna uwezekano wavunje mkataba wa kocha, tutafute kocha mwingine na pia turudi shuleni kusaka vipaji vya kuviendeleza, siku zote tusiishie kubabaisha," alisema Zungu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
Aliongeza kuwa endapo Tanzania itashindwa kuifunga Chad kwenye mechi zinazokuja za kuwania nafasi ya kuingia kwenye makundi ya kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, utakuwa ni wakati muafaka kwa viongozi wa TFF kujivua 'gamba' kwa kuachana na kocha huyo.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Fredrick Mwakalebela, aliliambia gazeti hili kuwa wachezaji walijituma kadri ya uwezo wao kuhakikisha kwamba wanashinda, lakini walizidiwa kiufundi na wapinzani wao ambao wana timu bora zaidi.
Mwakalebela alisema vilevile kuwa kiutawala, TFF haikuwa imeiandaa vizuri timu kufuzu fainali hizo ambapo alieleza kwamba hakukuwa na umakini wa kuwaita wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi mara zote kwa sababu imejidhihirisha kwamba hawakuwa wanafika kwa wakati ambao watafanya mazoezi ya pamoja na wenzao na kupokea maelekezo ya kocha.
"Timu haikupata mechi za nguvu za kujipima na tulizopata zilikuwa dhaifu, kambi haikuwa na hadhi, hapakuwepo na ahadi za kuwahamasisha wachezaji na wafadhili pia wamekaa kando sana," alisema Mwakalebela.
Aliongeza kuwa hamasa ya wananchi kwa timu yao haikuwepo kama ilivyokuwa wakati wa uongozi wake huku hamasa pia ya kuwataka wadau wasafiri na timu na Kamati ya Operesheni Ushindi kutofanya kazi yake ni sehemu ya mambo yaliyochangia kushusha morari ya wachezaji.
Nahodha wa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, Sophia Mwasikili, aliwataka wachezaji wa Stars wasikate tamaa na kuongeza juhudi zaidi ili washinde mechi zake mbili za kuwania nafasi ya kupangwa kwenye makundi ya kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Sophia alisema kuwa wanachotakiwa kukifanya wachezaji wa Stars kwa sasa ni kuangalia walipokosea ili wasirudie makosa hayo kwa sababu Watanzania wanaumia kuona timu yao haifanyi vizuri.
Saidi Motisha alisema kuwa ili mafanikio yapatikane, ni lazima maandalizi yawe ya muda mrefu na wachezaji wanaotoka nje ya nchi wafike mapema ili kupata mafunzo ya kocha kikamilifu.
Motisha alisema kwamba ushindi kamwe haupatikani kwa maneno na huu ni wakati wa kufufua programu za michezo shuleni na vyuoni ambako hutoa wachezaji wenye vipaji na kupatiwa mafunzo.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa wameyapokea matokeo hayo na sasa wanasubiri ripoti ya kocha ambayo itapitiwa na baadaye kutoa maamuzi kulingana na majukumu aliyopewa wakati anasaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.
Osiah alisema kuwa kuvunja mkataba wa kocha huyo kunahitaji sababu za kiufundi na vilevile Watanzania wanatakiwa kufahamu kwamba Poulsen peke yake hapaswi kulaumiwa kutokana na kushindwa kwa timu hiyo.
Stars inarejea nchini leo asubuhi na mechi yake ya kwanza dhidi ya Chad itachezwa Novemba 11 jijini Ndjamena, na ya marudiano itafanyika jijini Dar es Salaam Novemba 15.
MARRAKECH
Katika mechi ya juzi, Stars ilifungwa mabao 3-1 na Morocco katika mechi yao iliyochezwa kwenye uwanja uitwao ‘Grand Stadium’ na kushuhudia na maelfu ya watazamaji kwenye uwanja huo wenye viti 43,000. Hadi mapumziko, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji Morocco ndiyo waliotangulia kupata bao katika dakika ya 19, mfungaji akiwa ni Marouane Chamakh aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Adel Taarabt na mpira huo kudunda kabla ya kumpita kipa Juma Kaseja na kujaa wavuni.
Abdi Kassim aliisawazishia Stars katika dakika ya 40 kwa shuti kali la umbali wa mita 35 lililomshinda kipa Nadir Lamyaghri kufuatia pasi safi ya Idrissa Rajab.
Mabao mengine ya Morocco ambayo imepata tiketi ya kucheza fainali za AFCON zitakazochezwa mwakani katika nchi za Equatorial Guinea na Gabon yalifungwa na Taarabt katika dakika ya 68 na Mbark Boussoufa alipigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao la tatu katika dakika ya mwisho ya muda wa kawaida wa mechi hiyo.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha wa Stars, Poulsen, aliwataka wachezaji wake wasikate tamaa kutokana na matokeo hayo kwa vile walicheza na timu bora kuliko wao. Alisema hivi sasa wanatakiwa kuelekeza akili zao katika mechi mbili zilizo mbele yao dhidi ya Chad.
Katika hatua nyingine, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, ambaye ameambatana na timu hiyo nchini Morocco, amesema kuwa Stars itarejea jijini Dar es Salaam leo saa 2:30 asubuhi.
Mbali na Morocco, mataifa mengine yaliyofuzu fainali za CAN 2012 zitakazofanyika Januari 21 hadi Februari 12 na kuungana na wenyeji Gabon na Equatorial Guinea ni Angola, Botswana, Burkina Faso, Ghana, Guinea, Ivory Coast, Mali, Libya, Niger, Senegal, Sudan, Tunisia na Zambia.
CHANZO: NIPASHE

No comments: