ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 11, 2011

Utawala bora wampa Rais ubilionea wa kutupa


Rais Pedro Verona Pires wa Cape Verde, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya MO Ibrahim kwa viongozi wa Afrika wenye mafanikio kwa mwaka 2011.
Tuzo ya MO Ibrahim, ilianzishwa kwa lengo la kutambua na kutukuza uongozi bora kabisa wa Kiafrika, ambapo mshindi hupewa zawadi ya dola milioni tano za Marekani kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 mfululizo na baada ya hapo, hupewa dola 200,000 za Marekani kila mwaka kwa maisha yake yote.
Kadhalika, Mfuko wa MO Ibrahim, utafikiria kudhamini kiasi kingine zaidi cha dola 200,000 za Marekani kila mwaka kwa kipindi cha miaka 10 kwa ajili shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa kijamii. Akitangaza mshindi huyo wa mwaka huu (2011) wa Tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo, Salim Ahmed Salim, alisema:

“Kamati ya tuzo imevutiwa sana na mtazamo wa Rais Pedro Pires, katika kuibadilisha Cape Verde kuwa nchi ya kidemokrasia ya mfano, utulivu na kuongeza matumaini. Katika kipindi chake cha miaka 10 kama rais, taifa hilo limekuwa ni nchi ya pili kusherehekea kutoka kwenye nchi za mwisho kwa maendeleo za Umoja wa Mataifa na kushinda tuzo za kimataifa ya haki za binadamu na utawala bora.”
Salim Ahmed Salim alipongeza uwajibikaji wa kidemokrasia na utawala bora wa Rais Pires.
Alisema: "Heshima ya demokrasia ya Rais Pires, iliongezeka zaidi pale alipotangaza kuwa ataachia uongozi katika kipindi chake cha mwisho cha pili cha uongozi wake."
Akitupilia mbali ushauri kwamba Katiba ingebadilishwa kumruhusu awanie tena kuiongoza nchi yake. Alisema: "Hiki ni kitu rahisi cha utii kwa nyaraka zinazoliongoza taifa kwa sheria."
Katika uongozi wake, Rais Pires, amekuwa mtiifu kwa kuwatumikia wananchi wake, wakiwemo wanaoishi nje ya nchi (diaspora).
Tuzo ya Ibrahim ilianzishwa na Mfuko wa MO Ibrahim, ambao mwaka huu unaadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.
Mshindi wa tuzo hiyo huchaguliwa na Kamati ya Tuzo inayojumuisha watu mashuhuri saba.
Kamati ya Tuzo hutathmini na kumchagua kiongozi wa taifa wa zamani kutoka nchi za Afrika za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wametumikia vipindi vyao kulingana na katiba ya nchi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Baada ya kupata matokeo ya taarifa za mshindi wa tuzo hiyo, muasisi wa MO Ibrahim, alisema: “Ni ajabu kuona kwamba kiongozi wa Kiafrika aliyelitumikia taifa lake tangu wakati wa utawala wa kikoloni hadi kwenye demokrasia ya vyama vingi, wakati wote akiangalia maslahi ya wananchi wake na kulinda kanuni. Ukweli ni kwamba, Cape Verde na rasilimali zake kidogo, inaweza kuwa nchi ya kipato cha kati, ni mfano siyo tu kwa Bara la Afrika, bali pia kwa dunia. Rais Pires ni kiongozi anayestahili tuzo hii."
Hata hivyo, haikufahamika mara moja Rais Pires alishindanishwa na viongozi gani wa Afrika hadi akaibuka mshindi wa tuzo hiyo.
Alipoulizwa viongozi wengine walioshindanishwa katika kumpata mshindi wa tuzo hiyo, Afisa wa Mfuko huo, Dawn Rennie, alijibu kwa njia ya simu kutoka jijini London, Uingereza: “Kimsingi si utaratibu kuwataja viongozi wastaafu wa Kiafrika walioshindanishwa katika kupata tuzo hiyo."
Viongozi wengine waliowahi kutunukiwa tuzo ya MO Ibrahim kabla ya Rais Pires ni Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano (2007) na Festus Mogae (2008) wa Botswana. Mzee Nelson Mandela, alipata tuzo hiyo kwa heshima mwaka 2007.
Hata hivyo, mwaka 2009 na mwaka jana, baada ya Kamati ya Tuzo MO Ibrahim haikumpata mshindi yeyote.
CHANZO: NIPASHE

No comments: