ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 11, 2011

Mwanafunzi achomwa moto kwa tuhuma za kuiba kuku, Sh. 50,000


Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Laso, Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, ameuawa kwa kuchomwa moto kwa tuhuma za kuiba kuku na Sh. 50,000 kwenye nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Kileuo.
Tukio hilo la kikatili, lilitokea Oktoba 9, mwaka huu, majira ya saa 11:30 jioni.
Inadaiwa kuwa mtoto huyo (15-16) akiwa na wenzake watatu, walikwenda kuiba kwenye nyumba inayomilikiwa na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Joyce, ambako wanadaiwa kuiba kuku na fedha taslimu Sh. 50,000.

Habari za kuaminika zilizothibitishwa na Mtendaji wa Kijiji hicho, Gaudence Shayo, zinaeleza kuwa mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika shule hiyo na alikuwa mtoro wa muda mrefu.
“Sikuwapo wakati mtoto huyo anachomwa moto. Lakini nilifika nikakuta tayari ameshachomwa hadi kufa. Na nilipohoji, walidai kuwa alikamatwa akiiba. Alipokutwa na vitu alivyoiba, alikiri kuwa ameiba kwa kushirikiana na wenzake watatu, ambao wamekimbia, Na ndio wananchi walipompiga na kisha kummwagia mafuta ya taa na kumchoma moto,” alisema Shayo.
Alisema mtoto huyo, mwaka jana alikamatwa kwa tuhuma za kuiba kahawa debe mbili na kufikishwa katika Mahakama ya Mwanzo katika mji mdogo wa Himo.
Shayo alisema baada ya kesi hiyo kusikilizwa, alihukumiwa kwenda jela miezi sita, lakini kutokana na umri wake kuwa mdogo, viongozi wa kijiji hicho waliomba kumdhamini, asipelekwe jela ambapo wangesimamia aende shule.
Alisema baada ya kurejea kijijini humo, aliendelea na masomo ya darasa la nne, ambapo alikwenda shuleni kwa miezi mitano na kisha kurejea kwenye kazi yake ya wizi.
Shayo alisema mapema mwaka huu, alikamatwa na kufikishwa polisi kwa kosa lingine la wizi, lakini aliachiwa kwa kuhurumiwa kutokana na umri wake.
Alisema mtoto huyo, ambaye anaishi na bibi yake kutokana na wazazi wake kuwapo jijini Dar es Salaam, anadaiwa kushindikana kijijini humo kutokana na kujihusisha na wizi. Indaiwa kuwa mara kadhaa amefikishwa katika ofisi za kijiji hicho na kuonywa juu ya tabia yake, lakini hakubadilika.
Mmoja wa wananchi walioshuhudia tukio hilo, Joseph Assey, aliliambia NIPASHE kuwa mtoto huyo alikuwa mwizi wa siku nyingi na kwa siku hiyo, alikamatwa akiwa ameiba kuku na fedha kwa Joyce na alipohojiwa alieleza kuwa alikuwa na wenzake watatu amekimbia.
“Tulimkagua mtoto yule na kumkuta na Sh. 50,000. Amekuwa kero kwa muda mrefu. Watu kijijini hawaishi kwa amani. Alishotoroka kwa bibi yake na kwenda mahali pasipojulikana na kuonekana pale anapofanya uhalifu,” alisema.
Mtendaji wa Kijiji cha Lego Muro, ambacho kiko jirani na eneo la tukio, Adamu Mbuya, alisema kitendo kilichofanywa na wananchi hao si kizuri kwani walitaiwa kumfikisha katika nyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa na si kumchoma moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa hadi sasa hakuna anayeshikiliwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: