ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 11, 2011

Wabunge watatu waingia matatani


 Mmoja asomewa mashitaka kutishia kuua
  Wawili wakaripiwa na hakimu kortini
Modestus Kilufi
Wiki imeeanza vibaya kwa wabunge watatu kujikuta wakikabiliwa na msukosuko katika mahakama tofauti, wakati mmoja akishitakiwa kwa kutishia kuua, wengine wawili wakipewa onyo kali na hakimu kwa kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili.
Jijini Mbeya, Mbunge wa Mbarali (CCM), Modestus Kilufi (51), jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya na kusomewa shitaka la kutishia kudhuru.

Akimsomea mashtaka, Wakili wa Serikali, Griffin Mwakapeje, alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Machi 16, mwaka huu akiwa wilayani Mbarali, ambako alitishia kumdhuru Jordan Masweve.


Alidai kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa siku hiyo, ni kinyume cha kifungu cha 89, kifungu kidogo cha 2 (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16, kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Kilufi alikana mashtaka hayo.

Wakili Mwakapeje aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo akaomba ipangwe tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Kabla ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, anayesikiliza kesi hiyo hajataja tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, Wakili wa utetezi, Mwakolo, aliinuka na kumwombea dhamana mteja wake hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.

Hata hivyo, Hakimu Mteite aliagiza mtuhumiwa Kilufi kwenda mahabusu wakati mahakama ikiendelea kufikiria masharti ya dhamana kwa ajili yake, kisha akaiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 24, mwaka huu itakapoitishwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

ALALA RUMANDE
Mbunge huyo jana alilala rumande kutokana na mahakama kutokamilisha utaratibu wa kumpangia masharti ya dhamana. Baada ya kesi kuahirishwa, Kilufi alikuwa amewekwa chini ya ulinzi wa polisi na wakili wa upande wa utetezi alikuwa akihaha kukamilisha taratibu za dhamana kwa ajili ya mteja wake.

Kilufi alikamatwa na polisi Oktoba 7, mwaka huu, majira ya saa 10:30 jioni, akiwa ofisini kwake wilayani Mbarali na kusafirishwa chini ya ulinzi mkali kwenda katika kituo kikuu cha Polisi mjini Mbeya. 

Akiwa katika kituo cha Polisi Mbeya, Kilufi alilala rumande hadi majira ya saa 6:30 mchana Jumamosi Oktoba 8, mwaka huu, alipoachiwa kwa dhamana na kutakiwa kurudi kituoni hapo jana Jumatatu kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

WABUNGE WA CHADEMA WAPEWA ONYO
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, imewaonya wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutokana na kushindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili ya kumdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

Akitoa onyo hilo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, alisema mahakama inalazimika kutoa onyo kwa washitakiwa hao, Sylvester Kasulumbai (Maswa Mashariki) na Susan Kiwanga (Viti Maalum), kutokana na kutoridhika na sababu zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi.

Alisema kitendo hicho kinaonyesha washitakiwa hao wanajali kazi zao na kutotoa kipaumbele kwa mahakama.

Kutokana na hali hiyo, alisema kama hawatafika mahakamani tena, watafutiwa dhamana ili wakakae rumande.

Alihoji kama wasingelipata dhamana, je, mahakama ingewapa muda na ruhusa ya kuhudhuria vikao hivyo vya kamati?.

Hakimu Simba alienda mbali zaidi kwa kusema hata kama ni wabunge, wanatakiwa kuheshimu sheria za mahakama kwani chochote kinachotokea kinatakiwa kutolewa maelezo na sababu zinazowafanya kutokuhudhuria mahakamani, ikiwa ni pamoja na kuomba ruhusa, vinginevyo kesi hiyo haitaisha mapema

Awali, kabla ya onyo hilo, Wakili Mwandamizi, Mussa Kwikima, aliyewawakilisha washtakiwa hao, alidai kuwa Kasulumbai na Kiwanga, walishindwa kuhudhuria mahakamani kwa sababu wako kwenye vikao vya kamati za Bunge.

Wakili huyo alidai kuwa mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Anwar Kashaga, alishindwa kuhudhuria mahakamani kwa vile yuko Hospitalini Bugando, jijini Mwanza akipatiwa matibabu. Kashaga ni kiongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) mkoani Tabora.

Pamoja na kutoa maelezo hayo Kwikima aliomba radhi kutokana na wateja wake kutofika mahakamani na kuihakikishia mahakama hiyo kwamba, kosa kama hilo halitatokea tena katika kipindi kijacho cha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa upande wa mashitaka, Juma Masanja na Mugisha Mboneko, ambao waliieleza mahakama kwamba, hoja hizo hazitoshi kuifanya mahakama ikubaliane nao kwa sababu hazina vielelezo vyovyote kama inavyotakiwa kisheria.

Mshitakiwa wa nne katika kesi hiyo aliyeoongezwa katika mashitaka hayo Oktoba 4, mwaka huu, Robert William, alirudishwa rumande, baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni Sh. milioni tano, mali isiyohamishika na wadhamini wawili.

Washitakiwa hao wanashitakiwa kwa mashitaka matatu kila mmoja ikiwa ni pamoja na shambulizi la kudhuru mwili, kuiba simu ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya Sh. 400,000 na kumuweka chini ya ulinzi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, kinyume cha Sheria.

Hata hivyo, Kasulumbai anakabiliwa na shitaka lingine la kutoa matusi dhidi ya DC Kimario.

Awali washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, mwaka huu wakisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Simba.

Upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili Juma Masanja na Mboneko, ulidai kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Septemba 15, mwaka huu katika kijiji cha Isakamaliwa wilayani Igunga.

Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo  hadi Oktoba 24, mwaka huu.

Kundi la wanachama, mashabiki na viongozi wa Chadema mkoani Tabora lilifika mahakamani kufuatilia kesi hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: