Moses Mashalla, Arusha
WAGONJWA waliolazwa katika Hospitali ya Lutheran Medical Centre ya hapa, juzi walilazimika kutoka wodini mbio, baadhi yao wakiwa na dripu mikononi kunusuru maisha yao baada ya kuzuka moto.
Habari zilizopatikana hapa jana, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa 4.30 hadi saa 5.20 usiku.
Kwa mujibu wa habari hizo, hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), iliwaka moto baada ya kutokea mlipuko wa kikemikali kwenye chumba cha dawa.
Waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walizuiwa kuingia ndani ya hospitali hiyo kwa maelezo kuwa kulikuwa na shughuli za kuuzima moto huo wakati huo, wagonjwa walionekana wakitimua mbio kupitia lango kuu la hospitali hiyo.
Wagonjwa hao walikuwa wakiokoa maisha yao huku wengine wakiwa na dripu mikononi na baada ya kupata taarifa za moto huo, ndugu, jamaa na marafiki wakifika hospitalini hapo kwa lengo la kuwaokoa.
Hata hivyo, moto huo haukuleta madhara zaidi baada ya kudhibitiwa na kikosi cha zimamoto mkoani.
Baada ya kufanikiwa kuudhibiti moto huo ambao ulikuwa umeanza kusambaa kwa kasi ndani ya hospitali hiyo, baadhi ya watumishi wa zimamoto walionekana kuwa na furaha kutokana na kuudhibiti huku wakiwakejeli wale wanaotuhumu jeshi hilo... “Semeni sasa na leo kuwa tumechelewa kufika kuzima moto.”
Baadhi ya maofisa wa polisi, wafanyakazi wa Shirika la Umeme Mkoa wa Arusha (Tanesco) na watumishi wa Zimamoto mkoani hapa walionekana katika eneo la tukio wakifanya jitihada za kuuzima moto huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana na Mkurugenzi wa Huduma wa Hospitali hiyo, Sizya Simba chanzo cha moto huo ni kulipuka kwa baadhi ya dawa zenye kemikali zikiwamo za kufulia nguo za wagonjwa.
Simba alisema dawa hizo ziliwasili juzi hospitalini hapo. Alizitaja kuwa ni pamoja na Jx laundry detergent na silex 630.
Alisema mara baada ya kulipuka, moto ulishika kwenye mbao za chumba zilimokuwa zimehifadhiwa na kisha kuanza kusambaa taratibu kabla ya mtumishi mmoja kugundua tukio hilo na kuutaarifu uongozi wa hospitali.
Alisema hadi sasa bado hawajajua thamani ya mali zilizoteketea kwa moto na kwamba timu ya hazina hospitalini hapo inafanya juhudi za kubaini thamani yake.
Kuhusu sababu za kulipuka, Simba alisema uongozi wa hospitali hiyo unafuatilia kwa umakini tukio hilo ingawa alidokeza kwamba huenda ni kutokana na kuhifadhiwa kwenye joto kali na kushindwa kuhimili au zilikwisha muda wake wa matumizi.
No comments:
Post a Comment