ANGALIA LIVE NEWS
Monday, October 10, 2011
Wizara ya Fedha yajivua mzigo wa Dowans
Geofrey Nyang’oro
SAKATA la malipo ya Sh111 bilioni kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, linaonekana kuichanganya Serikali baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kuamua kutua mzigo huo akisema wizara yake haihusiki na malipo hayo.
Wakati Mkulo ambaye ni waziri mwenye dhamana ya malipo ya madeni ya Serikali akitua mzigo huo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alisema wizara inasubiri maelekezo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mkanganyiko huo wa mamlaka za Serikali unakuja kipindi ambacho tayari kumekuwa na shinikizo kutoka kwa wanaharakati wakipinga kuilipa mabilioni hayo kwa kutishia kufanya maandamano nchi nzima, huku Chadema nayo ikitangaza kuwaunga mkono.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jijini Dares Salaam jana, Waziri Mkulo alisema wizara yake haihusiki na deni hilo na ndio sababu haikushirikishwa katika kila hatua zinazohusu uingiaji wa mikataba na hadi kuvunjwa kwake.
“Mimi na wizara yangu ya fedha hatuhusiki na malipo ya Dowans, ndio sababu hata mikataba hatukuingia sisi wala hatukushiriki. Zaidi hata nakala ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhusu kesi hiyo ya madai sijaiona,”alisema Mkulo.
Mkulo alikazia msimamo huo alisema, “Wanaohusika ni Tanesco, ndio walioingia mikataba na pia kuivunja na ndio waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Migogoro ya Kibiashara (ICC)”.
“Wizara ya fedha haihusiki na mikataba ya Dowans, wapo waliohusika. Lakini, katika suala la umeme sisi tunatafuta namna ya upatikanaji wa umeme wa kutosha ili kuwaondolea kero ya umeme wananchi,”alisema Mkulo.
Kauli ya Wizara ya Nishati na Madini
Maswi alisema tungu kutolewa kwa hukumu hiyo wizara yake imekuwa ikisuburi taarifa kutoka kwa AG ili iweze kutoa tamko.
Maswi alisema mara ya kupata taarifa hiyo, wizara itatoa tamko kuhusu hukumu hiyo.
“Hata sisi tumesikia suala hilo, lakini bado tunasubiri statement (taarifa) kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Yeye ndiye aliyekuwa akishughulikia suala hilo kwa niaba ya Serikali, atakapotupatia tutaandaa taarifa yetu na kuwapatia,” alisema Maswi.
AG Werema asema ni suala la kisheria
Kwa upande wake AG Fedrick Werema alipoulizwa juu ya suala hilo alisema kwa kifupi, “Ikiwa Mahakama imeshatolea uamuzi hilo kwa sasa ni suala la kisheria”.
“Kama Mahakama imeshaamua hilo ni suala la kisheria,”alisisitiza na kisha akakata simu.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment