Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
*JK awakubalia CUF kwenda Ikulu
SIKU moja baada ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 kutiwa saini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na msimamo mpya kikisema hakitashiriki hatua yoyote ya kuandika katiba iwapo Rais Jakaya Kikwete, ataruhusu sheria hiyo kutumika kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kabla haijarudishwa kwa wananchi ili ijadiliwe na kufanyiwa marekebisho.
SIKU moja baada ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 kutiwa saini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na msimamo mpya kikisema hakitashiriki hatua yoyote ya kuandika katiba iwapo Rais Jakaya Kikwete, ataruhusu sheria hiyo kutumika kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kabla haijarudishwa kwa wananchi ili ijadiliwe na kufanyiwa marekebisho.
Msimamo huo wa Chadema, ulitangazwa na Kaimu Katibu Mkuu wake, John Mnyika, alipozungumza na waandishi wa habari, kufafanua mambo yaliyoibuka baada ya kamati iliyoundwa na vigogo wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti taifa, Freeman Mbowe, kukutana na Rais Kikwete na ujumbe wa serikali yake, kwa siku mbili mfululizo Ikulu, kuanzia, Novemba 28, mwaka huu na kufikia makubaliano.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Katibu wa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema iwapo Rais Kikwete hataruhusu sheria hiyo kufanyiwa marekebisho, makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo yao, hayatakuwa na maana.
Alisema katika mazungumzo hayo, pande zote mbili ziliona sheria hiyo kuwa ina upungufu, hivyo inahitaji kuboreshwa.
Mnyika alisema baada ya kuona kwamba kuna haja hiyo, walimshauri Rais Kikwete, kutumia mamlaka yake ya Kikatiba kutosaini muswada wa sheria hiyo, lakini ushauri wao huo umepuuzwa.
Hata hivyo, alisema pamoja na kupuuza ushauri wao wa kutokusaini, Rais Kikwete amekubaliana kwamba kuna haja ya kuboresha sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa mwito wa kupeleka maoni juu ya marekebisho hayo.
“Hivyo, tunataraji Rais hataunda tume ya kukusanya maoni mpaka atakapokamilisha mchakato wa sheria hiyo kufanyiwa marekebisho. Na hii italeta maana ya makubaliano tuliyofikia,” alisema Mnyika.
Aliongeza: “Kabla sheria haijaanza kutumika, irudishwe kwa wananchi ili watoe maoni.”
Akielezea sababu za pande mbili za mazungumzo kukubaliana kuwapo mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo, Mnyika alisema walizingatia jambo hilo kwa vile Katiba ni mali ya Watanzania.
Alisema kama wasingefikia makubaliano hayo, wangekuwa wamefanya makosa yaliyofanywa na serikali kwa kujifungia ndani na kutengeneza muswada wa sheria hiyo na kisha kuupeleka bungeni bila kuwashirikisha wananchi.
Alisema miongoni mwa vipengele wanavyopinga kuwamo kwenye sheria hiyo, ni pamoja na kinachohusu uanzishwaji wa Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kutoa maoni juu ya rasimu ya katiba.
Mnyika alisema sheria hiyo inakataza mtu yeyote kufanya shughuli ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi au kuendesha elimu juu ya mabadiliko ya Katiba, ambapo alisema adhabu kwa yeyote atakayetiwa hatiani kwa makosa hayo, ni faini ya kati ya Shilingi milioni tano hadi Sh. milioni 15 au kifungo cha kati ya miaka mitatu hadi saba au vyote kwa pamoja.
Alisema masharti hayo ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana madhara makubwa sana sio tu kwa mchakato wa utungaji wa Katiba Mpya, bali pia kwa haki za kibinadamu na za kikatiba zinazotambuliwa na kulindwa na Katiba na sheria za nchi pamoja na sheria za kimataifa, ambazo Tanzania imeziridhia.
Kuhusu sheria hiyo kuanza kutumika leo, alisema jambo hilo siyo lazima, kwani hata mwaka 1984, Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusaini sheria, lakini ilianza kufanya kazi baada ya miaka mitatu.
Alisema pia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010, haikuanza kufanya kazi ila baada ya kufanyiwa marekebisho.
Kutokana na hayo, alitangaza rasmi msimamo wa Chadema akirejea azimio la sita la Kamati Kuu ya Chadema iliyofanya kikao chake Novemba 20, mwaka huu, linalosema kwamba ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kupata katiba mpya uliowekwa na sheria hiyo, utategemea utayari wa serikali kufanya mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.
Hivyo, akasema: “Chadema hatutashiriki mchakato wowote unaotokana na sheria hiyo iwapo haitafanyiwa marekebisho.”
Alisema pia kutokana na makubaliano waliyofikia katika mazungumzo na Rais Kikwete, wamesitisha maandamano, lakini hawajasitisha kazi za chama kuhusu mchakato wa suala la katiba.
Mnyika alisema Chadema wataendelea kutoa elimu juu ya ubovu wa sheria hiyo kwa kufanya mikutano ya ndani na hadhara. “Tunataraji serikali italeta katika Bunge lijalo marekebisho ya sheria hiyo kwa kuzingatia maoni ya wananchi,” alisema Mnyika.
JK KUKUTANA NA CUF
Wakati huo huo, Ofisi ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema kuwa Rais amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza maandalizi ya mkutano huo yafanyike mara moja.
CHANZO: NIPASHE www.ippmedia.com
No comments:
Post a Comment