Aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo hivi sasa inayojulikana kama TBC ll Taifa, David Wakati, alizikwa jana katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Misa ya kumuombea marehemu ilifanyika katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Alban ambapo Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk.Valentino Mokiwa, aliongoza sala ya kumuombea marehemu na kusema kuwa atakumbukwa na Watanzania wengi kwa ucheshi wake na mchango alioutoa katika tasnia ya habari.
“Katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru kama historia ya utangazaji itaandikwa, hakika jina la David Wakati halitakosekana katika sura zake nyingi kwa mchango mkubwa alioutoa,” alisema mmoja wa wanafamilia wakati akisoma historia fupi ya marehemu
Aidha, misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na watu mashuhuri, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa zamani, Jaji Mark Bomani; Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame; Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi; Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Paul Rupia.
Marehemu Wakati alifariki dunia Desemba Mosi, 2011 katika hospitali ya Regency na ameacha watoto watatu, ambao ni Mandela Kenneth, John Kuchi na Steve Biko.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment