ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 2, 2011

Gari la kigogo CCM lanasa mtoni kwa saa 4-Habari Leo

Mkazi wa Iramba akihatarisha usalama wake kwa kuingia chini ya gari la Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi, Mwigullu Lameck Nchemba kulinasua gari hilo lililokuwa limekwama kwenye mto Ndurumo Kata ya Kidaru Mkoani Singida. (Picha na Abby Nkungu)

KATIBU wa Uchumi na Fedha wa CCM-Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mwigullu Lameck Nchemba, ameonja adha ya barabara mbovu baada ya gari lake kukwama mtoni na kulazimika kutumia saa 4 kulinasua. 

Katibu huyo ambaye alikuwa amefuatana na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Singida, Mhandishi Frank Kisanga, walikuwa kwenye ziara ya siku moja ya kukagua miundombinu ya barabara katika jimbo la Iramba Magharibi. 

Barabara hizo ni pamoja na ile iliyopandishwa hadhi na kuwa ya mkoa inayoanzia Kiomboi mjini - Kisiriri - Kidaru. 

Gari hilo la Mwigullu lilikwama kwenye mto Ndurumo katika kijiji cha Ndurumo kata ya Kidaru wilayani Iramba. 

Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser GX 8 lilinasuliwa na wananchi wa kijiji cha Ndurumo na hivyo kuendelea na ukaguzi wa barabara ya Kidaru - Doromoni hadi Shelui. 

Akizungumza na waandishi wa habari,mbunge huyo, amewataka makandarasi kujenga/kukarabati barabara zinazofanana na thamani ya fedha zinazotumika na si vinginevyo,ili ziweze kudumu kwa muda mrefu. 

Katika hatua nyingine, Mwigullu alisema Sh milioni 89.5 zilizotengwa kwa kazi ya ukarabati wa barabara ya Kiomboi – Kisiriri – Kidaru, hazitoshi. 

Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali iangalie upya uwezekano wa kuiongezea fedha barabara hiyo ambayo inapitika kwa taabu karibu kipindi chote cha mwaka. 

Naye Kisanga alisema tayari zabuni ya kukarabati barabara ya Kiomboi–Kisiriri–Kidaru imeishatangazwa na makandarasi wamekwishakuomba. Kinachosubiriwa ni kuzifungua tu ili kazi iweze kuanza.

No comments: