WIKI iliyopita, nilipokea ujumbe mfupi wa maandishi wa simu (SMS) ambao ulisomeka hivi: “Halloo Brother Luqman, mimi naitwa Zabron A. Msindaki wa Iringa. Swali langu ni je, ninawezaje kuimudu simu ya mkononi bila kugombana na mchumba wangu?”
Swali kama hilo, lilitoka kwa Justina Alphonce wa Tegeta, Dar es Salaam ambaye aliuliza: “Mimi ni mwanamke, nipo kwenye ndoa kwa mwaka wa tatu sasa, lakini kila siku ugomvi kati yangu na mume wangu upo kwenye simu.
“Wakati mwingine, mimi ndiye chanzo, lakini mara nyingi ananiudhi. Kimsingi tunaoneana sana wivu, kwa sababu imefikia kipindi kila nikipiga au kupokea simu ni lazima ajue nimeongea na nani.
“Nikituma au kupokea sms, anataka ajue niliyemtumia au imetoka kwa nani, nilichoandika au kuandikiwa. Na kama ni simu wakati mwingine anapendelea niongee kwa ‘loud speaker’. Je, nifanyeje Mr. Luqman Maloto, ili na mimi niwe na amani kama wengine?”
Wakati hao wakiuliza, msomaji wangu, Jasmin Mdanzi wa Mwanza, SMS yake ilisomeka: “Kaka yangu Luqman Maloto, naomba utuandikie mada inayohusu masuala ya simu za mkononi na suluhisho lake.
“Maana ya kuomba hivyo ni kuwa kwa sasa mimi sina haja kabisa ya kumiliki simu ya mkononi. Najua umuhimu wake katika mawasiliano, lakini naikataa kwa sababu ya kuhofia kuvunjika kwa uhusiano na mpenzi wangu.
“Simu ni muhimu, lakini mpenzi wangu ni muhimu zaidi, sasa kwa nini itutenganishe? Imeniletea matatizo makubwa, boyfriend wangu anahisi namsaliti, kitendo ambacho kinanikosesha amani kabisa.”
Msomaji wangu, hizo ni SMS tatu kati ya nyingi ambazo nimewahi kutumiwa, zikiongelea matatizo anuwai yaliyopo nyuma ya matumizi ya simu za mkononi.
Ni kupitia ‘meseji’ hizo, ndiyo maana nikaona, niteue somo la leo, liwe linahusu utandawazi hasa wa simu za mkononi na kile kinachotokea kwenye mitandao ya kijamii, nikiamini kwamba hapo nitakuwa naenda sawa na wasomaji wangu.
Twende kwenye pointi; si kwa mtu mmoja au wawili, bila shaka utakuwa umeshashuhudia wapenzi wakitengana, wanandoa wakikosa suluhu kwa sababu ya SMS au simu. Baadhi wapo katika uhusiano wa ‘ilimradi siku zinaenda’, yaani ni mashaka tupu.
Kama si upande huo wa shilingi, basi utakuwa umeshajionea jinsi watu wanavyokosa amani mbele ya wapenzi wao. Wakizima simu muda wote au wakiishia kuwapiga marufuku wasiziguse kwa kuhofia siri zao kugundulika.
Unadhani hayo ndiyo mapenzi? La hasha! Wawili wanaopendana, ni sharti kati yao kuwe na amani, upendo, uaminifu na uhuru wa kila mmoja kwa mwenzake. Wanaowekeana mipaka, hao wamepata alama ‘F’ katika taaluma ya ‘malavidavi’.
Inawezekana hata upande huo ukawa ni mgeni kwako, lakini huu utakuwa unaujua. Ipo Kasumba ya baadhi ya watu kutunza namba za simu za wapenzi wao wa pembeni kwa majina tofauti.
Wanawake ‘kusevu’ majina ya kike, wakati wanaume wakiwaandika wenzi wao wa nje kama wanaume wenzao. Husna kuitwa Hussein, Nasra kuandikwa Nassor au Jane kama John.
Wanawake nao, Joseph kuandika Josephine, Justin kuita Justina au kumuandika Ramadhan kama Swaumu. Umenipata? Hayo ndiyo mapenzi ya kileo na balaa lililopo katika simu za mkononi.
Dunia inavyopanuka ndivyo mambo ya utandawazi yanavyoshamiri. Simu za mkononi zilitikisa lakini kwa sasa Facebook inatajwa kwa sana. Kuna watu sasa hivi wanaishi roho juu kila wakijua wapenzi wao wapo ‘online’. Kuna jamii inaanzisha uhusiano mpya kila siku.
Nikiwa online katika ukurasa wangu wiki iliyopita, kuna ndugu mmoja aliniuliza: “Luqman, hujaona jinsi Facebook inavyohamisha mapenzi. Watu wanaanzisha uhusiano mpya kila siku mtandaoni. Hali ilivyo, Facebook inapunguza kiwango cha uaminifu.”
Ni hoja inayohitaji uchambuzi wa kina. Ipo wazi kwamba Facebook inagusa mitima ya idadi kubwa ya watu. Na sipingani na mtazamo wa rafiki yangu kuwa kuna watu wanashinda mitandaoni kuwinda wapenzi badala ya kukuza mtandao wa maisha, biashara na kadhalika.
Kuna vijana wanatumia muda wao mtandaoni kusaka wanawake wakubwa ili walelewe. Lipo kundi la ‘wadada’ wanaohangaikia mabwana wa nje hususan Wazungu. Mtu ana mpenzi wake lakini anaanzisha urafiki na baadaye mapenzi baada ya ‘kuchati’ naye mara kadhaa. Maendeleo yamekuja na mambo leo!
Itaendelea wiki ijayo…
www.globalpublishers.info
2 comments:
Kaaaazi kweli kweli....!
sio mchezo kazi aswaaa wanaume wenyewe ni washezi .na mambo yamebadilika siku hizi ukiweza kumkomesha lijimwanaume komesha tu akuna mpole wala mzee wala mtoto.
Post a Comment