Baada ya kufanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi uongozi wa timu ya Azam FC umesema kwamba zama za Simba na Yanga kuongoza soka la Tanzania zimepitwa na wakati na sasa wanaelekeza nguvu zote katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza Jumamosi Januari 21.
Uongozi huo umesema kuwa kutokana na kuibuka klabu zenye uwezo mkubwa wa kusakata soka, timu hizo zitaondoka katika utawala wa soka hapa nchini kinyume na matarajio ya Watanzania wengi.
Hayo yameelezwa na Kiongozi Mwandamizi wa Klabu hiyo, Salum Bakharesa katika hafla fupi ya kuipongeza iliyofanyika makao makuu ya klabu ya Malindi Zanzibar hivi karibuni.
“Moto tulioonyesha katika kombe la Mapinduzi pia utaendelea kuwaka katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara,”alisema Kiongozi huo kuwa timu yake inataka kufikia lengo la kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo tangu kuanzishwa mwaka 2003.
Bakhresa alisema kuwa timu hiyo imeonyesha kiwango cha hali ya juu katika mashindano hayo na wanamiini kuwa kiwango hicho wataendelea kukionyesha katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Hata hivyo alisema kwamba mafanikio yaliyopatikana kwa timu hiyo yametokana na ushirikiano mkubwa waliopata kutoka kwa wanachama na washabiki wa timu hiyo tangu yalipoanza masindano hayo Januari 2 mwaka huu.
“Kazi kubwa iliyombele yetu ni kuona Azam inafikia malengo yake ya kunyakuwa ubingwa wa soka Tanzania Bara kama ilivyotokea Kombe la Mapinduzi,”alisema Bakharesa.
Alisema kwamba kitendo cha wapenzi wa timu hiyo kuwa karibu tangu kuanza kwa mashindano hayo kulisaidia kuwapa moyo wachezaji na viongozi na hatimaye kufikia malengo yao.
Upande wake, Katibu Mkuu wa Malindi, Ali Majjid alisema kwamba ushindi wa Azam wameupokea kama ushindi wa timu yao ya Malindi kutokana na ushirikiano mkubwa uliyopo kati ya klabu hizo.
Aidha, alisema kwamba siri ya kombe hilo kunyang’anywa Simba imetokan na viongozi wa Azam na Malindi kufanya kazi bega kwa bega tangu kuanza mashindano hayo mwaka huu.
Timu za Simba na Yanga zilishindwa kumaliza safari ya mashindano ya kuwania kombe la Mapinduzi baada ya kushindwa kuingia hatua ya fainali kwa kutolewa na Azam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment