ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 10, 2012

Chadema yaitikisa Arumeru

CHAMAcha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kilizindua rasmi kampeni za ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki kwa kishindo cha aina yake. 

Uzinduzi wa kampeni hizo ulianza kwa maandamano makubwa yaliyojumuisha magari, 
pikipiki na umati wa wananchi huku Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema akiwa juu ya gari lake akipunga mikono. 


Awali ilidaiwa Lema alipigwa marufuku kugusa Arumeru kwa madai ya kuwakashifu wazee wilayani humo. 

Maandamano hayo yalinza saa mbili asubuhi na ilipofika saa 5 asubuhi idadi ya watu magari na 
pikipiki iliongezeka maradufu hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari kwa watumiaji wa barabara kuu ya Moshi – Arusha. 

Mbunge Lema akiwa katika gari lake hilo alikuwa akionesha ishara ya kukata shingo hatua iliyokuwa ikiwafanya wafuasi wa chama hicho kushangilia kwa nguvu. 

Kabla ya kuanza mkutano wa uzinduzi, helikopta ya Chadema ilikuwa ikionesha mbwembwe 
mbalimbali angani na kuwasisimua washiriki wa mkutano huo ambao walishangilia kwa 
nguvu huku ndani mwake kukiwa na mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho, Joshua 
Nassari, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi kadhaa. 

Mkutano huo ulifunguliwa na viongozi wa dini, ambao walisisitiza amani itawale katika Jimbo la Arumeru Mashariki na uchaguzi ufanyike kwa amani na hatimaye wananchi wachague mtu ambaye atawafaa. 

Pamoja na Nassari, Mbowe na Lema, viongozi wengine wa Chadema waliopambisha uzinduzi 
huo ni Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Kabwe Zitto, Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph 
Mbilinyi ‘Sugu” na Mkuu wa Ulinzi wa Chadema Wilfred Lwakatare. 

Akizindua kampeni hizo, Mbowe alihoji matumizi ya fedha zaidi ya Sh milioni 220 alizodai 
CCM ilitumia kwenye kura za maoni za kumpata mgombea wa jimbo hilo na alimuomba Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa majibu. 

Alisema Chadema ilitumia Sh milioni 6.2 tu kwa ajili ya chakula kwa wajumbe wa chama hicho na kuendesha gharama za uchaguzi. 

Alisema kisheria gharama za uchaguzi zinatakiwa zisizidi Sh milioni 80. 

Alihoji Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema kupeleka magari ya kuwasha, askari, mabomu na silaha kwa wingi wilayani humo huku akisema Chadema ni chama cha kistaarabu ambacho hakihitaji fujo. 

Naye Nassari, alitaka watu wanaotaka asichaguliwe kwa kuwa hajaoa wapuuzwe, huku 
akisema kuoa ni mipango ya Mungu na kwamba muda ukifika ataoa. 

Alitoa mfano kuwa Bunge lina watu mahiri kama Mnyika, Sugu na wengine ambao hawajaoa, lakini wanatimiza vyema majukumu yao. 

Wakati Chadema wakizindua kampeni, leo ni zamu ya TLP inayoongozwa na Augustine Mrema 
wakati kesho CCM inatarajiwa kuanza kumnadi mgombea wake, Siyoi Sumari, huku kampeni 
zake zikizinduliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Habari Leo

No comments: