Sioi Sumari akiwa amebebwa na wafuasi wa chama chake CCM
WANANCHI wa Jimbo la Arumeru Mashariki, wameombwa kumchagua mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia CCM, Sioi Sumari ili kumfuta machozi yaliyotokana na kifo cha baba yake mzazi, Jeremiah Sumari ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo.
Mbali na hilo wananchi hao wameelezwa kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wamejipatia baraka kwa Mungu kwani watamwezesha Sioi kupata mshahara utakaomwezesha kuendesha familia aliyoachiwa na baba yake.
Mwito huo ulitolewa juzi katika Kijiji cha Migadini, Kata ya Mororoni na Mbunge wa Mtera(CCM), Livingstone Lusinde alipokuwa akimnadi mgombea huyo katika kampeni za uchaguzi mdogo zinazoendelea jimboni humo.
Lusinde alisema wananchi hao wanastahili kuwa na moyo wa huruma kwa kumchagua kwa kura nyingi ili ajipatie mshahara wa kumwezesha kumudu familia aliyoachiwa na marehemu baba yake, ikiwa ni moja ya njia ya kumfuta machozi.
“Mkimchagua Sioi mtapata baraka za Mungu kwa vile mtakuwa mmewezesha kutokea kwa mambo matatu… kwanza kura zenu zitamfuta machozi ya kufiwa na baba yake, pili mtamwezesha kupata mshahara utakaomwezesha kulea familia yake ambayo sasa haina baba,” alisema Lusinde.
Pia aliwaambia wananchi hao kwamba kumchagua Sioi kuwa mbunge wa jimbo hilo ni kumfurahisha Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa huyo ndiye chaguo lake na ndiye aliyeongoza vikao vya Kamati Kuu iliyokutana mara mbili kupitisha jina lake kuwa mgombea wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Alisema katika kura hizo za maoni zilizofanyika mara mbili, zote Sioi alionekana kushinda na kuibuka kidedea.
“Njia pekee ya kumfurahisha Rais ni kumchagua Sioi kwa kuwa ni chaguo lake, hakika mtamfurahisha na Sioi ataweza kutekeleza vyema ilani ya chama,” alisema Lusinde.
Kwa upande wake, Sioi alisema anayaelewa vyema matatizo yanayoikabili Kata ya Maroroni ikiwemo ukosefu wa mashamba ya uhakika, maji, barabara na zahanati hivyo akichaguliwa, atayatatua matatizo hayo mara moja.
“Nawaombeni sana mnichague kuwa mbunge wenu ili kwa pamoja tuweze kushirikiana kutatua kero hizi ambazo kimsingi zote nazifahamu vyema na nafahamu pia hatua za kuchukua ili kuhakikisha tunaondokana nazo,” alisema Sioi.
Shabiki wa Chadema
Katika tukio jingine hekima na busara za Mratibu Mkuu wa kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba zilitumika kuepusha maafa kwa mwanachama mmoja wa Chadema, aliyevalia sare za chama hicho baada ya kufika kwenye mkutano wa CCM katika Kata ya Kikatiti.
Wakati Mwigulu akihutubia mkutano huo, mwanachama huyo wa Chadema, ghafla alivamia mkutano huo na kuanza kupiga mayowe huku akitamka maneno ya "Peoples Power" (Nguvu ya umma).
Hatua hiyo iliwakera wafuasi wa CCM ambao waliamua kumtia adabu kabla ya Mwigulu kuingilia kati kuwazuia akiwataka wamwache kwani alikuwa anapaswa kufundishwa sera za CCM.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment