ASKARI Polisi wameendelea na utovu wa nidhamu licha ya onyo la Rais Jakaya Kikwete
baada ya mmoja kutimuliwa kazi kwa ukosefu wa maadili ikiwemo ulevi huku mwingine akishitakiwa katika Mahakama ya Kijeshi kwa tuhuma za kumshusha mbunge katika mkutano
wa hadhara kabla ya muda wa kibali kuisha.
Rais Kikwete akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro hivi karibuni, alionya kuhusu kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu kwa askari wa jeshi hilo vikiwemo vya ulevi, kupiga wananchi na wanalalamikiwa kwa kuendekeza rushwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema jana kuwa Koplo Alistide amesimamishwa kazi na kushitakiwa katika Mahakama ya Kijeshi kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Koplo Alistide ambaye pia ni dereva gari la Polisi katika Kituo Kikuu cha Mpanda, anadaiwa
kuvamia mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Pudensiana Kikwembe (CCM) na kumshusha kwa nguvu.
Akizungumza na gazeti hili, Dk. Kikwembe alikiri kushushwa jukwaani na askari huyo Machi 4,
mwaka huu katika Kijiji cha Kakese na kusema awali alipovamiwa, alidhani ni raia wa kawaida aliyekuwa amekunywa pombe.
“Kwanza nilijua ni mwananchi wa kawaida ametoka amechangamka (amelewa), lakini kumbe
alikuwa ni askari, mimi nilimsamehe isipokuwa ni jukumu la Jeshi la Polisi kulinda nidhamu ya askari wake sababu muda ulikuwa bado haujafika kuufunga mkutano wangu huo kwa mujibu wa kibali walichonipa wenyewe polisi,” alisema Mbunge huyo kutoka Mkoa mpya wa Katavi.
Inadaiwa askari huyo alipanda jukwaani alipokuwapo mbunge huyo akihutubia na kumwamuru ashuke jukwaani mara moja vinginevyo angeanza kumshughulikia ipasavyo.
Kwa mujibu wa madai hayo, mbunge huyo akiwa ameshikilia kipaza sauti alimsihi askari huyo
huku akimwonesha kibali cha mkutano kuwa muda uliokuwa umeruhusiwa, ulikuwa haujawadia, lakini askari huyo hakutaka kumsikiliza.
Inadaiwa askari huyo aliwaamrisha wenzake kufunga mkutano, lakini walimkatalia kwa kumsihi aache vurugu.
“Ilimlazimu mbunge huyo kufunga mkutano kwa kutumia kipaza sauti kuwatangazia wananchi waliokuwa wamehudhuria mkutano huo wa hadhara,” alidai mtoa taarifa wetu.
Kamanda Mwaruanda alisema vitendo kama hivyo vya utovu wa nidhamu havivumiliki katika Jeshi hilo na hatua za nidhamu zimeshachukuliwa dhidi ya askari huyo ikiwamo kufunguliwa mashitaka ya kijeshi.
Alisema askari huyo alikosa nidhamu na kujichukulia sheria mikononi mwake na kuonesha
utovu wa nidhamu wakati mkubwa wake wa kazi alikuwepo katika eneo hilo la tukio na ndiye alipaswa kuwasiliana naye.
Kuhusu kama askari huyo alikuwa amelewa pombe na kufanya fujo, Kamanda Mwaruanda alibainisha kuwa ni vigumu kusema moja kwa moja kwani ni lazima uthibitishe hilo ingawaje matendo yake yalikuwa yakiashiria hali hiyo, lakini hakufanya fujo yoyote isipokuwa alichofanya ni utovu wa nidhamu.
Mkoani Manyara, nako askari Polisi wa Idara ya Upelelezi wa Kituo cha Polisi Mirerani katika
Wilaya ya Simanjiro amefukuzwa kazi kwa kosa la kupiga risasi matairi ya matrekta mawili
yaliyokuwa yanakwenda kulima wilayani Kiteto mkoani humo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Liberatus Sabas alithibitisha jana kufukuzwa kwa askari huyo aliyetajwa kwa jina moja la Nathanael wa Kituo cha Polisi Mirerani.
Mtoa taarifa wetu, alidai kuwa Nathanael alifukuzwa kazi kutokana na kitendo chake cha
kupiga risasi matairi ya trekta zilizopita pembeni ya kituo hicho cha Polisi yakienda shambani.
Alidai trekta hizo zilikuwa zikitoka eneo la Ngarenairobi katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kwenda wilayani Kiteto mkoani Manyara kwa ajili ya kulima mashamba kwa kukodishwa.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, baada ya matrekta hayo kupigwa risasi, madereva hao waliwasiliana na mmiliki wake ambaye aliitaarifu Polisi.
“Bosi huyo wa Polisi alipiga simu mara moja kwa mmoja wa madereva wa matreka hayo
aliyekuwa kituo cha Mirerani na kumtaka ampe simu askari huyo Nathanael ambaye alizimia baada ya bosi huyo kujitambulisha kwake,” alidai mtoa taarifa wetu.
Alidai usiku huo huo, Nathanael alikamatwa na kulala mahabusu kwa muda wa siku tatu kwa amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mirerani (OCS), Elisha Saenda na baada ya muda wa siku kadhaa alifukuzwa kazi.
Mwaka juzi, askari Polisi wa Kituo cha Orkesumet makao makuu ya wilaya hiyo ambaye
alikuwa analinda benki ya NMB Tawi la Orkesumet, alifukuzwa kazi baada ya kupiga risasi hewani bila sababu ya msingi.
Inadaiwa askari huyo alivuta bangi na kulewa na kuanza kupiga risasi hewani bila sababu yoyote na kutishia watu waliokuwa karibu na eneo hilo huku akitaka kuonana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Mkuu wa Polisi (IGP).
Imeandikwa na John Mhala, Mirerani na Peti Siyame, Sumbawanga.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment