ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 18, 2012

Mahakama ya Kadhi yaibuka tena bungeni

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana alilazimika  kuingilia kati kujibu swali kwa ajili ya kutuliza mzimu wa Mahakama ya Kadhi ulioibuka bungeni.

Pinda aliingilia kati suala hilo na kulitolea ufafanuzi jambo hilo ili kuondokana na kuwepo kwa mgawanyiko wa wabunge ambao wanataka Mahakama ya Kadhi kinyume na sheria ya nchi.  Aidha, alisema jambo hilo linatakiwa kutazamwa kwa umakini mkubwa kulingana na hali halisi ya nchi na mwisho wake lipatiwe mwafaka.

“Jamani naomba niwaambie ndugu zangu wabunge jambo hili naona linavuta hisia ya watu wengi kwani linagusa imani za watu, lakini nataka kuwaambia jambo hili halitaki haraka ni lazima kwenda nalo kwa umakini mkubwa, lakini serikali ilishaunda timu ya pamoja ya viongozi wa dini ya Kiislamu na serikali kwa ajili ya kuongelea jambo hili na hata juzi tulikaa kikao na tuliweza kuongea.”
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed ambaye aliitaka serikali isema kwa kwa nini imekuwa na kigugumizi kutoa maamuzi ya kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi kama zilivyo kwa nchi nyingine za Uganda, Msumbiji, Zanzibar na nyinginezo.

Pia Mbunge huyo amehoji kuwa nchi inaongozwa kwa Sheria hivyo ni sheria ipi ambayo inayoruhusu dini ya Kiislamu  kuanzisha Mahakama hiyo.
Mbunge huyo alisimama kutokana na majibu ya Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, kujibu swali la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habibu Mnyaa (CUF).
Katika swali lake la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali haijaona umuhimu wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi ambayo ndiyo yenye mamlaka kamili kwa imani ya dini ya Kiislamu kutoa tafsiri sahihi ya mirathi, ndoa au talaka.
Akijibu swali hilo, Waziri Kombani, alisema wanajamii wa dini husika wanatakiwa kuanzisha mahakama yao bila kuishirikisha serikali na kuongeza kuwa utaratibu wa unatakiwa kufanywa na dini husika bila kuihusisha serikali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: