ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 20, 2012

Marufuku kuwawekea alama wanafunzi wanaoishi na VVU


Serikali imesema itazipiga marufuku baadhi ya shule kuwawekea alama nyekundu begani wanafunzi ambao wana matatizo ya kiafya wakiwemo wanaoishi naVirusi vya Ukimwi (VVU) kwa kuwa ni kinyume na haki za binadamu.
Hayo yalisemwa jana na Afisa Tawala na Mratibu wa Masuala ya jinsia na Ukimwi  kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Joyce Mlowe alipokuwa akizungumza katika mjadala wa uwekaji wa alama nyekundu kwa watoto wenye matatizo ya kiafya, wakiwemo wanaoishi na virusi vya ukimwi uliondaliwa na Baraza la Taifa la  watu wanaoishi na virusi vya ukimwi (NACOPHA).
Mlowe alisema Wizara baada ya kupata taarifa hizo ilishtushwa na kuridhia mikataba mbalimbali ya  sheria za Kimataifa ya  haki za binadamu na kulaani kitendo hicho kinachofanywa na baadhi ya shule za msingi katika Wilaya ya Kibaha na kuwaathiri wanafunzi hao kisaikolojia.
Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Peter, alisema  mapema Machi, 2012 walisikia taarifa kwa vyombo vya habari juu ya wanafunzi kuwekewa alama nyekundu wilayani Kibaha na kulifuatilia.
Alisema  kitendo hicho kililikera baraza hilo kwa vile ni unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wenye matatizo ya afya hasa watu wanaoishi na VVU, wakafuatilia na kubaini kuwa alama hizo zimechangia watoto hao kuwa tofauti na wengine kitu kilichopelekea kutengwa na wengine.

Alisema utafiti wilayani Kibaha wa uwekewaji alama kwa wanafunzi hao ilibainika kuwa ni maamuzi ya wazazi na walimu kwa lengo la kuwatambua ili wasipangiwe kazi ngumu na wasipewe adhabu.
Aidha alisema Baraza hilo limetoa mapendekezo yao kuwa uwekaji alama nyekundu unadhalilisha haiba na uhuru wa mtoto shuleni na katika jamii na kutaka upigwe marufuku kwa kuwa madhara yake ni makubwa.
Wakili wa Kituo cha  Sheria na Haki za  Binadamu (LHRC), Harold Sungusia, alilaani kitendo hicho kwa kuwa watoto wanastahili kuwa na masilahi bora na wanatakiwa kulindwa, kutunziwa siri na hawatakiwi kunyanyapaliwa wala kubaguliwa.
Sungusia alizitaka wizara husika ikiwemo ya Afya,Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Halmashauri ya Kibaha na uongozi wa shule hizo kupiga marufuku kitendo hicho  kwa kuwa sheria inawatambua.
CHANZO: NIPASHE

No comments: