ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, April 24, 2012
Ubingwa Simba waingia kwikwi
Mshambuliaji wa timu ya Simba, Emmanuel Okwi (kulia) akipambana na mchezaji wa timu ya Moro United, Omari Gae wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Simba ilishinda mabao 3-0. (Picha na Yusuf Badi).
LICHA ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Moro United lakini ndoto za Simba jana
kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu 2011/2012 ziliingia kwikwi baada ya mechi ya Azam na Mtibwa Sugar iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, kuvunjika.
Mechi hiyo ilivunjika baada ya wachezaji wa Mtibwa Sugar kugomea penalti iliyotolewa na mwamuzi wa mechi, Rashid Msangi wa Dodoma kwenye dakika ya 88 ya mchezo huo, wakati timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
Kwa hali hiyo kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka nchini (TFF), timu itakayovunja
mechi itapokwa pointi tatu na kupewa timu pinzani, hali inayochelewesha sherehe za ubingwa za Simba kwani Azam ambayo jana ilifikisha pointi 53 ina uwezo wa kufikisha pointi 59 zilizofikiwa na Simba kama itashinda michezo yake miwili iliyobaki dhidi ya Kagera Sugar na Toto Africans.
Ili Simba ijihakikishie kutwaa ubingwa inatakiwa kushinda mechi yake ya mwisho Mei 5 dhidi ya Yanga ambapo itakuwa imefikisha pointi 62 au ifikishe pointi 60 kwa kutoka sare, lakini ikifungwa, bingwa itabidi aamuliwe kwa tofauti ya mabao kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Kwenye mchezo wa jana dhidi ya Moro United, mabao ya Simba yalifungwa na kiungo
wa pembeni wa timu hiyo, Uhuru Selemani kwenye dakika ya 6 kabla ya kuongeza bao la pili katika dakika ya 10 lililofungwa na kiungo Patrick Mafisango kwa mkwaju wa penalti baada ya mabeki wa Moro kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili.
Katika mchezo huo timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa kwa Simba kuwatoa Shomari Kapombe, Selemani na Gervas Kago na nafasi zao kuchukuliwa na Nassoro Masoud, Salumu Machaku na Felix Sunzu, huku Moro ikiwapumzisha Hilal Bingwa na Benedict Ngassa na nafasi zao kuchukuliwa na Kelvin Charles na Simon Msuva.
Mabadiliko hayo yalionekana kuinufaisha zaidi Simba kwani waliandika bao la tatu kupitia kwa Sunzu katika dakika ya 73 akiunganisha kwa kichwa krosi nzuri ya Emmanuel Okwi kutoka upande wa kushoto wa uwanja.
Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment