VURUGU zilizotokea juzi mjini Ikwiriri wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, zimesababisha watu 50 kufikishwa mahakamani wakishitakiwa kwa makosa mbalimbali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Ernest Mangu aliliambia gazeti hili jana kuwa wamewafikisha watu hao kwa tuhuma za kufanya vurugu, kupora kwa kutumia silaha na kuiba mifugo.
Kamanda Mangu alisema makosa ya watuhumiwa hao yanatofautiana kutokana na sehemu alikokamatwa mtu na tukio lilifanyika eneo hilo.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekamatwa wakiwa na nyama ya ng’ombe, hali inayoonesha kuwa walienda kuvamia maboma ya wachungaji na kupora mifugo na kuichinja, jambo ambalo alisema ni kosa kisheria.
Alisema wameshuhudia vichwa vitatu vya ng’ombe ambao wameuawa na watuhumiwa hao, hivyo waliohusika na kosa hilo wameshitakiwa kwa kosa la kuvamia, kuiba kwa kutumia silaha. Pia alisema watuhumiwa wengine wamekamatwa kwa makosa ya kubomoa maduka na kupora kwa kutumia silaha.
Alisema kuna maduka mawili yaliyokuwa yanauza dawa za mifugo yamebomolewa mjini Ikwiriri hivyo watuhumiwa waliokamatwa katika eneo hilo wanashitakiwa kwa kosa hilo.
Pia alisema kuna nyumba nane zimevunjwa na watuhumiwa ni miongoni mwa watuhumiwa hao 50 ambao nao wamefungulia mashitaka kulingana na kosa hilo.
Kamanda Mangu alikanusha kuwa hakuna nyumba yoyote iliunguzwa moto, bali alisema waliokamatwa wengi ni vijana ambao ndio ambao wamezusha vurugu hizo baada ya kupata taarifa za mkulima kuuawa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafugaji.
Alisema tuhuma kuwa watu wa jamii ya wafugaji walimuua mkulima, sio za kweli, bali mtu aliyekumbwa na mauti hayo, Shamte Twangala alikufa wakati akikimbizwa na kutumbukia kwenye korongo.
Alisema ni kweli kuwa mtu huyo aligombana na vijana wawili wa jamii ya wafugaji baada ya kuingiza mifugo katika shamba lake na wakati wakiwa katika majibizano, mzee huyo wa makamu aliogopa na kuanza kutimua mbio.
“Wakati anakimbia akatumbukia shimoni na kwa kuwa alikuwa na mshono, hali yake ikawa mbaya zaidi, lakini hata uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa hakuuawa kwa kupigwa,” alisema kamanda huyo wakati akizungumza na gazeti hili kwa simu.
Akielezea hali ilivyo kwa sasa, kamanda huyo wa polisi alisema hali ni shwari ila jana muda wa saa nne asubuhi kulitokea purukushani wakati walipokuwa wanawapeleka watuhumiwa mahakamani.
“Ila kwa sasa tunavyoongea hali ni shwari na tunaendelea kuwasaka viongozi walioshawishi kuzuka kwa vurugu hizo,” alisema kamanda huyo.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment