ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 22, 2012

Mapenzi ni bahati, kama ulipo si bahati yako, endelea kutafuta

YALIANZA kuumbwa maisha halafu mapenzi ndiyo yakafuata. Aliumbwa Adam, baadaye akaletewa Hawa kisha mapenzi ndiyo yakaanza. Hii ina maana kuwa maisha yalianza kwa upande wa Adam kabla ya mapenzi. Hili zingatia katika kutafsiri sura ya kule uendako maishani.
Hata wewe jiulize, ulipozaliwa ulikuwa hujui mapenzi ni nini? Hapa sizungumzii mapenzi ya kawaida, yale ambayo mtu anaweza kuyapata kutoka kwa wazazi wake au ndugu zake wengine. Yanayotajwa hapa ni mapenzi katika maana yake halisi. Mapenzi ya ndani kabisa.
Yale ambayo huwafanya watu waziache familia zao za asili na kwenda kutengeneza nyingine. Nayazungumzia yale ambayo yanawafanya watu wanauana, wengine wanakunywa sumu. Yanayowatesa watu mpaka wanashindwa kula na kadhalika.
Swali ni moja; Kama iliwezekana kuishi bila mapenzi mpaka ulipofikisha umri wa utu uzima, iweje leo yakutawale mpaka ushindwe kujiendesha mwenyewe? Haipingiki kwamba mapenzi ni muhimu lakini hayapaswi kutawala ubongo wako. Utafeli haraka.
Mapenzi ni mazuri kwako endapo utaweza kuyamudu. Yakikushinda wewe ni mtumwa. Kaa, tuliza akili halafu tafakari. Baada ya hapo chukua hatua. Haijalishi umeshaathirika kiasi gani, muhimu kwako ni kuzingatia kwamba inawezekana kubadilika.
Japo unapenda mno, unajitahidi kuonesha unajali katika mazingira yoyote. Umemfanya mwenzako sawa na mboni yako kwa namna unavyomtunza. Kama yeye harudishi mapenzi unayompa, hajali na kukupa heshima kulingana na ile unayompa, angalia maisha yako kwanza.
Angalizo; Ukimng’ang’ania sana, atakugeuza punda. Atajipa kiburi kwamba anaweza kufanya lolote nawe utatii kwa sababu unampenda. Usidanganywe na imani zisizokuwepo, binadamu hawekwi kiganjani wala kwenye chupa. Una akili hai, tazama mbele pengine hapo si kwenye bahati yako.
Kama anashindwa kukuthamini kwa namna unavyompenda, hawezi kuyapenda maisha yako. Atakutumia atakavyo, akishatimiza malengo yake na kukuacha ukihangaika na dunia. Wakati huo yeye yupo na mtu wake anayempenda, atakuwa anakenua na kukucheka.
Akikaa na marafiki zake, atawaambia kwamba yeye ndiye alikuwa nyota yako, kwamba ulipokuwa naye maisha yako yalikuwa rahisi na hivi sasa umechoka baada ya kuachana naye. Hatazungumza jinsi alivyokutesa, akakuweka roho juu, akakusababishia maumivu ya moyo mpaka ukashindwa kutekeleza majukumu yako.
Usikubali muda wako upotee bure. Maisha yako ni ya thamani, yupo nawe leo lakini kesho inawezekana si wa kwako lakini maisha yatabaki kuwa yako kwa mazingira yoyote yale. Hoja yangu hapa ni kwamba mapenzi yasikutawale mpaka ukasahau maisha.
Wengi waliishia njiani, walijiaminisha wanapendana kutoka ndani ya kuta za nyoyo zao. Wakaahidiana kuwa hakuna kitakachowatenganisha. Siku yalipotimia, ahadi zote zikayeyuka. Hupaswi kung’ang’ani ulipo, bali yafaa ujiulize, je, hapo ndipo kwenye bahati yako?
Watu kwenye ndoa wameachana, si kwamba walipenda la hasha! Wachumba wanaishia njiani, vilevile marafiki walioamini wanachanua, wakapeana mkono wa kwa heri. Ni vizuri kukubali kwamba jitihada hazishindi kudura. Pamoja na mapenzi yako makubwa, unavyojali, unavyomheshimu kama si bahati yako hamuwezi kudumu.
Haijalishi utu wako ni wa thamani kiasi gani. Mzee Nelson Mandela ‘Madiba’, alitoa talaka kwa bibi yetu, Winnie. Waliishi miaka mingi, wakazaa watoto ambao wengine kwa sasa ni wakubwa kabisa. Baadaye akagundua Winnie si bahati yake, leo yupo kwenye ndoa na Graca Machel, maisha yanaendelea.
Kumbe Graca ndiye bahati ya Mzee Mandela. Ilivyo ni kwamba Winnie alitangulia kwa lengo la kukamilisha safari ya maisha ya babu yetu huyo anayeheshimiwa mno duniani. Chukua mfano huo, halafu jipe matumaini. Maisha ni matamu mno bila ya huyo wako ambaye si bahati yako.
Napenda tena nitie mkazo kwamba mapenzi ni magumu. Kama Mandela yalimuumiza, inashindikana vipi kwako? Ukimpata wa bahati yako, hata uwe maskini unaweza kung’ara na maisha yako yakatawaliwa na faraja, ila ukitumbukia sehemu ambayo si yako, ni mateso ya moyo na sononeko lisilokwisha.
Hapa nifafanue kuwa yule ambaye anajiona yupo kwenye uhusiano salama, basi aendelee hapohapo kwa sababu ndipo kwenye bahati yake. Kwa wale wenye maumivu pale walipo, basi wajiangalie mara mbilimbili. Maisha yanaendelea. Maisha bora yanajengwa na mtu mwenye akili iliyotulia.
Huwezi kuwa na matatizo, akili haitulii kwa sababu ya misukosuko ya kimapenzi, ukadhani kwamba utajenga maisha imara. Hapo utakuwa unajidanganya. Tibu kwanza janga lako la mapenzi ili maisha yako yanyooke. Ikiwezekana, jipe muda wa kukaa ‘singo’. Inawezekana.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers,info

3 comments:

Anonymous said...

hii nzuri sana articles nimeipenda sana na imenielimisha sana nikweli mtu usinganganiye mapenzi kama hakuna bahati yako unayempenda asiyekupenda kama unavyompenda haina maana hata kidogo kuwa katika uhusiano huu japo kuwa ni ngumu sana kumsahau na kutoa akilini lakin inawezekana take one step a day at a time au vipi poa sana hii shukran vijimambo kwa kutupa hii kitu poa na very informatives
mdau aliye gushwa na penzi kama hili na anaye teseka lakin sasa kaona nuru ya mwaka anajitoa

Anonymous said...

Jamani akishajua unampenda ndio basi tena, vituko vinaanza mara simu hakupigii, mara aseme hawezi kukuona, kuanzisha ubishi usio na kichwa na miguu. Karaa tele kunyanyasa roho yako

Anonymous said...

Wengi tumeteseka ktk mapenzi, tatizo ni kwamba watu wanasahau mambo fulan kuwa ni kiungo na gundi ya mapenzi. Mapenzi hayana mazoea, yaani kuwa Romantic. Ndio inayosababisha ndoa/wapenzi kusalitiana. Na kuwa busy mno na majukumu mengine na kusahau kabisa kama mwenzi wako aliye nyumbani anakusubiri. Mawasiliano matamu hata upo kazi au safarini. Mwanzo wa mapenzi utaitwa maneno yooote matamu na msg nzuri za mapenzi, siku zinavyozidi mwenda hayo yote yanapotea taratibu.
Kwa ufupi ni kuwa Romanti life kwa wapenzi hakuna.