ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 24, 2012

Shibuda sasa amvaa Dk Slaa,adai kuwatumia Bavicha

Aidan Mhando
MSUGUANO wa vijana wa Chadema (Bavicha) na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki , John Shibuda, umezidi kuongeza joto la kisiasa ndani ya chama hicho  baada ya mbunge huyo kumrushia kombora Katibu  Mkuu, Dk Willibrod Slaa, akisema ndiye anayewatumia vijana hao kumhujumu.


Tayari Shibuda ameigawa Bavicha baada ya Mwenyekiti wake, John Heche kupingana hadharani na makamu wake, Juliana Shonza kuhusu msimamo wa baraza hilo dhidi ya hatua ya mbunge huyo kutangaza dhamira ya kuwania urais mwaka 2015 ndani ya Nec ya CCM na kumwomba Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete awe kampeni meneja wake. 

Wakati kauli zake hizo ndani ya Nec ya CCM zikitarajiwa kumweka katika hatari ya kufukuzwa ndani ya Chadema kipindi hiki ambacho amekuwa katika uangalizi maalum, Shibuda jana aliliambia Mwananchi kwamba, yuko tayari kwa lolote na wakati wowote tena kwa asilimia 100.

Shibuda alifafanua kwamba anatuhumiwa kukihujumu chama huku akiwa hajawahi kukiuka maagizo yoyote ya Kamati Kuu ndani ya Chadema , lakini amebaini  kuna baadhi ya watu wanatumiwa na viongozi wa juu wa chama hicho akiwamo Dk Slaa kwa lengo la kumfanyia fitina na hujuma.

Alisema kitendo cha Dk Slaa kukalia kimya shutuma zinazoelekezwa kwake na vijana hao wa Chadema kinampa fursa ya kuamini kwamba vigogo wa chama hicho wako nyuma yao na kumtaka sasa Dk Slaa aeleza hadharani uovu wake huo ili Watanzania wafahamu ukweli kuhusu sakata hilo.

"Mimi sina kosa lolote ila ninachofikiria ni kwamba Bavicha wanatumiwa na viongozi wa juu wa Chama ili kutaka kuniharibia lakini cha msingi ni vyema Katibu Mkuu wetu (Dk Slaa), akaweka hadharani maovu yangu ili Watanzania wajue makosa yangu ni yapi," alisema Shibuda na kuongeza:
"Ni wakati wa Chadema kupitia viongozi wake wakuu  kueleza ubora wake wa kuwaongoza wananchi uko wapi kwani kama mtu anatangaza nia na kuonekana ameenda kinyume, sidhani kama kuna uongozi thabiti."

Kitisho cha  kufukuzwa
Akizungumzia kitisho cha kuweza kufukuzwa Chadema,  Shibuda alisema  kwa sasa yupo tayari kwa asilimia 100 kupokea  jambo lolote litakalotokea dhidi yake ndani ya chama hicho na kwamba kinachotakiwa ni kuonyeshwa makosa yake.

"Kwa asilimia 100, kutoka moyoni nasema nipo tayari kwa lolote litakalotokea kwangu ndani ya Chadema, kwani mimi natambua wazi  sina kosa nililolifanya na kama nina makosa basi yaanikwe hadharani ili wananchi nao watambue," alisema.

Akizungumzia kupewa barua ya karipio kali,  Shibuda alisema kwamba, hata siku moja hajawahi kupewa barua yoyote ya karipio kali na hafahamu chochote juu ya suala hilo.

"Sikiliza ndugu mwandishi, mimi sijawahi kupewa barua yoyote ya karipio kali na sifahamu chochote juu ya suala hilo labda hao walionipa barua hiyo wangeeleza lini walinipa," alisema.  

Kauli ya Dk Slaa/ Heche
Akizungumzia tuhuma hizo za Shibuda,  Dk Slaa alisema asingependa kuingizwa katika mjadala huo kwani hajawahi kumzungumzia Mbunge huyo kuhusu jambo lolote wakati wowote tangu mjadala wake na Bavicha ulipoanza.

Alisema haoni suala la Shibuda kama ni jambo la kuzungumzia kwa sasa kwani halina msingi na kuna mambo mengi ya kujadili ili kuliwezesha taifa kupambana na umasikini.

"Mimi nisingependa kuhusishwa na suala la Shibuda kwani sijawahi kuzungumza chochote kumhusu yeye na kwamba, nina mambo mengi ya kuangalia na sio Shibuda," alisema Dk Slaa na kuongeza:
"Sipendi kuzungumzia kauli za watu hata kidogo kwani tunakazi kubwa ya kupambana na kuwakomboa wananchi kutoka katika umasikini."

Heche, akizungumzia tuhuma hizo kwamba Bavicha inatumiwa  kumhujumu Shibuda, alisema hawezi kuzungumzia suala la Shibuda sasa kwa kuwa tayari kuna vikao vimeanza kukaa kulijadili.
Alisema baada ya kukamilika kwa vikao vya Kamati tendaji ya Bavicha, watatoa majibu sahihi yanayohusu masula mbalimbali ya vijana, lakini pia watatoa ufafanuzi na msimamo wao kuhusu Shibuda.
“Tuna vikao ambavyo vinaanza kesho (leo) na  baada ya kumalizika ndipo tunaweza kutoa ufafanuzi kuhusu mambo yote tutakayojadili ikiwa ni pamoja na msimamao wetu kuhusu Shibuda,” alisema Heche.

Matukio yake
Hi ni mara ya tatu kwa Shibuda kuingia katika mgogoro wa ndani ya chama kwani, mara ya kwanza aliwahi kukiuka msimamo wa wabunge wa Chadema kutoka nje ya ukumbi wa bunge kwa kupinga matokeo yaliyompa Kikwete Urais badala yake usiku alihudhuria dhifa maalumu Ikulu ndogo Chamwino baada ya mkuu huyo wa nchi kuzindua Bunge la kumi.

Shibuda pia aliwahi kuingia katika mgogoro na chama hicho kutokana na msimamo wake wa kuendelea kupokea posho za bunge na kutaka ziongezwe hadi kufika Sh500,000, akiziita "ujira wa mwiha," huku akirusha vijembe kwa baadhi ya wabunge wenzake akisema ni wafanyabiashara siyo wabunge jamii. 
Matukio hayo yalimfanya aundiwe Kamati Maalumu chini ya Profesa Abdalla Safari kwa lengo la kuangalia nyendo zake na matokeo yake, ni kuwa chini ya uangalizi maalum ndani ya miaka miwili kuanzia sasa vinginevyo CC imfukuze lakini, ameibua mjadala mwingine wakati hata mwaka huo wa uangalizi maalumu haujakamilika.

Katika sakata hilo la sasa tayari kumeibuka mvutano ndani ya Bavicha baada ya Shonza kupinga tamko la Heche ambapo Mei 20, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema,  “Naomba ifahamike kwamba tamko alilolitoa Heche siyo la 

Baraza, bali ni lake kama Heche. Alipokuwa akitoa tamko hilo hakukuwa na kikao chochote cha Baraza cha viongozi wa kitaifa wala Sekretarieti ya Baraza la Vijana la Chadema ili kulijadili suala hili kwa kina bali, alitumia mwamvuli wa vijana kuhalalisha hoja yake.”

Hata hivyo, siku hiyo ya jioni Heche naye alitoa taarifa kwa umma akisema,  “Nimejulishwa kuwa Makamu wangu (Shonza), leo (Mei 20) amezungumza na vyombo vya habari na kukanusha taarifa niliyotoa kwa niaba ya Bavicha.

Itambulike kuwa majukumu na mamlaka ya mwenyekiti na kiongozi mwingine yeyote wa Baraza yanabainishwa na Kanuni za Baraza letu kifungu 5.4.1, ambayo mwenyekiti ndiye msemaji mkuu wa Baraza na pia ndiye kiongozi mkuu wa Baraza katika ngazi husika.”


Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

chadema we need to get together and shut this punk down ,because i think ametumwa ,he trying to change the direction of our maendeleo ship direction
mtz washington dc usa