ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 25, 2012

Aliyepasuliwa kichwa badala ya mguu adai Sh1 bil

Daniel Mjema
KIJANA Emanuel Didas ambaye alifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu katika hospitali taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (MOI), ameishitaki Serikali akiidai fidia ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Kesi hiyo namba 159/2012 imefunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na ndugu wa Didas anayejulikana kwa jina la Sisti Marishay Alhamisi iliyopita baada ya kupata idhini ya mahakama (Power of Attorney) ya kumwakilisha ndugu yake huyo.

Katika kesi hiyo inayosubiri kupangiwa Jaji atakayeisikiliza, Didas ameishitaki Bodi ya Wadhamini ya MOI ikiwa ni mdaiwa wa kwanza, Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akiwa mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mdaiwa wa tatu.

Katika hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani Marishay anadai kuwa, Oktoba 26, 2007 ndugu yake huyo alipata ajali ya pikipiki Barabara ya Bagamoyo, jijini Dar Es Salaam na kupelekwa katika kitengo hicho (MOI).

“Alipofikishwa hapo alilazwa na kuchukuliwa vipimo ikiwamo X-Ray na kubainika amevunjika mfupa wa mguu wake mmoja na hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa damu iliyoganda,”anadai Marishay.

Katika hati hiyo iliyowasilishwa mahakamani na Wakili Cornelius Kariwa kwa niaba ya mdai, imedai kuwa Novemba mosi mwaka huo (2007), madaktari bingwa wakamfanyia Didas upasuaji wa kichwa badala ya mguu.


Imedaiwa kuwa madaktari hao bingwa walikiuka kanuni zote za kitabibu na utawala (SOPs) za kufanya upasuaji kwa kuchanganya majina ya wagonjwa wakati wa kufanya upasuaji siku hiyo.

Marishay aliyepewa idhini hiyo ya kisheria, amedai kuwa ndugu yake alikuwa mtu aliyejiajiri kama fundi makanika na alikuwa akiingiza kipato cha Sh25,000 kwa siku.

“Kutokana na madhara yaliyotokana na upasuaji huo, Didas amepata hasara ya Sh9,125,000 kwa mwaka kuanzia November 2007, hivyo anahitaji kufidiwa fedha hizo,” amedai Marishay.

Alidai kuwa uzembe wa kiwango cha juu katika upasuaji huo umemfanya Didas pia kuwa tegemezi akilazimika kumuajiri msaidizi kwa mshahara wa Sh150,000 kwa mwezi kuanzia mwezi Oktoba 2010.

Mdai katika kesi hiyo anaiomba Mahakama Kuu kuwaamuru wadaiwa kumlipa fidia ya jumla ya Sh950 kwa kumsababishia ulemavu wa kudumu, riba ya asilimia saba na kulipa gharama za kesi hiyo.

Pia anaiomba mahakama kuwaamuru wadaiwa kulipa fidia maalumu ya Sh9,125,000 kwa mwaka kuanzia Novemba 2007 na Sh150,000 za mshahara wa msaidizi kuanzia Oktoba 2010.

Kwa kiwango cha Sh9,125,000 cha fidia kwa mwaka, kuanzia Novemba 2007 hadi Novemba 2012, Didas atakuwa anadai fidia maalumu ya Sh45.6 milioni na misharaha ya msaidizi Sh3.1 milioni.

Didas aliyetakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu baada ya kupata ajali lakini akafanyiwa upasuaji wa kichwa huku mgonjwa mwingine aliyepaswa kufanyiwa upasuaji wa kichwa akapasuliwa mguu.

Kwa sasa Didas ambaye alifanyiwa upasuaji huo Novemba 1,2007 na madaktari bingwa wa kitengo cha mifupa (MOI) cha hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),amepooza upande wa kulia wa mwili wake.

Marishay alidai kuwa baada ya kuboronga kwa madaktari hao bingwa, ndugu yake alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Indraprastha Appolo nchini India ili kujaribu kuokoa maisha yake.

Kutokana na utata huo, MOI liunda Tume kuchunguza sakata hilo la madaktari bingwa kuchanganya majina ya wagonjwa wawili, Didas na Emanuel Mgaya (Marehemu), aliyepasuliwa mguu badala ya kichwa.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliikataa taarifa ya tume hiyo na kuunda tume nyingine chini ya daktari bingwa wa mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando Profesa William Mhalu.

Baada ya kukamilisha uchunguzi huo, Tume ya Profesa Mhalu ilibaini kuwa watabibu wa MOI walikiuka kanuni zote na kuwa wazembe katika kutimiza majukumu yao siku ya upasuaji wa Didas.


Mwananchi

No comments: