ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 25, 2012

Minziro aanza kusaka kikosi cha kwanza


Sweetbert Lukonge
KOCHA msaidizi wa Yanga, Fred Minziro, amesema viwango walivyoonyesha wachezaji wake wapya kwenye mazoezi bado havijamridhisha na kwa sababu hiyo, anatarajia kuwapima kwenye mechi kadhaa za wiki hii, ambapo pia atapata fursa ya kuunda kikosi cha kwanza.
Yanga, mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Kagame inayotarajia kuanza mwezi ujao jijini Dar es Salaam, imesajili wachezaji kadhaa akiwamo beki aliyejiunga toka Simba, Kelvin Yondani.
Minziro anatambua ugumu wa michuano ya Kombe la Kagame, hivyo kipimo cha nyota wake wapya ni mechi za kirafiki ambazo anakusudia kuomba toka kwa uongozi wake.
Akizungumza na Mwananchi jana, Minziro alisema kwa sasa anafanya mazungumzo na uongozi ili kuona kama anaweza kupata fursa ya mechi za majaribio kabla ya mashindano ya Kagame.
"Nina kikosi kizuri, wachezaji wote wameonyesha uwezo mkubwa, lakini bado nahitaji mechi kadhaa za kirafiki ili kujiweka sawa na michuano ya Kagame," alisema Minziro.
"Kuanzia wiki ijayo (wiki hii) natarajia kikosi changu kuanza kucheza mechi za kirafiki ikiwa ni moja kati ya mikakati yetu tuliojiwekea kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kagame na Ligi Kuu.

"Natarajia mechi hizo ndizo zitakuwa kipimo kwa wachezaji wote wa zamani na wale tuliowasajili msimu huu ili kuweza kupata kikosi cha kwanza," alisema Minziro beki wa zamani wa timu hiyo ya Jangwani.
Alisema, kwa kuwa tarehe za kuanza kwa michuano hiyo inakaribia, angependa kupata mechi hizo wiki hii ili kubaini makosa kama yatakuwapo.
Kuhusu mazoezi ya timu yake, Minziro alisema yanaendelea vizuri na anachofanya kwa sasa ni kuwaandaa wachezaji wake namna ya kukaa na mpira muda mrefu.
Hatua hiyo inafuatia baada ya wiki iliyomalizika wachezaji hao kufanya mazoezi magumu kwenye Uwanja wa Kaunda unaomilikiwa na klabu hiyo.
Aliongeza kwa kusema, wachezaji wote wanatambua wajibu wao kwenye mazoezi jambo ambalo limeifanya kazi yake kuwa rahisi.
"Kweli nimeridhika na namna wachezaji anavyojituma kwa ajili na mazoezi, siyo wale wa zamani wala wapya, wote wameonyesha uwezo mkubwa," alisema Minziro.
Baadhi ya wachezaji wapya Yanga waliosajiliwa mpaka sasa ni pamoja na Frank Domayo,  Simon Msuva, Said Banuzi, Ali Mustafa na Ladislaus Mbogo.

No comments: