ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 25, 2012

Kagasheki asimamisha vigogo 10 Maliasili


Waziri wa Mali Asili na Utalii Balozi Kagasheki akiteta jambo na Naibu wake
Boniface Meena na Mussa Juma
VIGOGO 10 waliokuwa wanatuhumiwa kwa ubadhirifu kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), katika Wizara ya Maliasili na Utalii wamesimamishwa kazi.
Operesheni hiyo safisha inaendeshwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye amethibitisha kuwa vigogo hao wamesimaishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.
Waliosimamishwa wametambuliwa tu kwa vyeo vyao, ni Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Matumizi ya Wanyamapori, Mkurugenzi wa Leseni na Uwindaji, Mkurugenzi wa Uwindaji, Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Wanyamapori, Ofisa Mfawidhi Kituo cha Cites na Uwindaji Arusha.
Wengine ni Ofisa wa Kituo cha Utafiti Arusha, Kaimu Mfawidhi wa Cites Arusha, Ofisa wa Uwindaji na Utalii Arusha pamoja na ofisa mmoja wa makao makuu, kitego cha Cites na Uwindaji.


Kabla ya kusimamisha vigogo hao, tayari Balozi Kagasheki alianza kwa kuwasimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori, Boneventura Tarimo na Ofisa Wanyamapori Mkuu, Mohamed Madehele.
Balozi Kagasheki alisema juzi kwamba waliosiamishwa wanachunguzwa na wakithibitika kufanya ubadhirifu watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu.

“Ni kweli wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Wakibainika watachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisema Kagasheki.
Ripoti ya CAG
Kusimamishwa kwa maofisa na wakurugenzi hao kunatokana na ubadhirifu uliotajwa na CAG katika ripoti yake ya mwaka uliopita, kitendo kilichosababisha aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Ezekiel Maige kung’olewa katika nafasi hiyo kwenye mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete Mei 4 mwaka huu.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa hiyo ilipoteza Sh874,853,564 kutokana na kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrahaba kwa mauzo ya misitu.
Maige pia alishutumiwa kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ambao inadaiwa ulitawaliwa na dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha ni vitalu vipi walivyopewa.

Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilieleza kuwa kampuni 16 zilizopewa vitalu hivyo hazikuomba na kwamba, vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili. 

Mbali na tuhuma hizo, Maige hivi karibuni alidaiwa kununua nyumba kwa dola 700,000 za Marekani katika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa nyumba hiyo ameinunua kwa dola 410,000, sawa na zaidi ya (Sh600 milioni).

Mwananchi

No comments: