ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 23, 2012

Bajeti ya Serikali yapita kwa mikwara


Bajeti ya Serikali imepita huku wabunge wa upinzani wakiipinga na baadhi ya wabunge wa CCM wakionyesha msimamo wa kuikataa tangu awali na wengine wakiingia mitini muda mfupi kabla kura kupigwa.
Luhaga Mpina (CCM), ambaye alionyesha kuikataa bajeti hiyo tangu awali alitoka muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji kura kwa kuitwa majina mmoja baada ya mwingine.
Kabla ya kutoka nje, Mpina alionekana akijadiliana jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) na baada ya hapo hakurejea tena kwenye kiti chake.
Mwingine aliyepinga bejeti hiyo katika michango yao lakini hakuwepo wakati wa upigaji wa kura ni Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) pamoja na Kangi Lugola (CCM, Mwibara).

Mbunge pekee wa upinzani aliyepiga kura ya ndio kuikubali bajeti hiyo ni John Cheyo, wa Baridi Mashariki (UDP), wakati Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alipinga bajeti hiyo kwa kusema hapana.
Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini  kuwa kulikuwa na mawasiliano baina ya Mpina na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira.
Mawaziri hao walionekana wakiwa wamekaa na Mpina kwenye viti viwili pamoja ambavyo vimewekwa kwenye lango kuu linalotumiwa na maofisa wa serikali na waandishi wa habari.
Hata hivyo, Waziri Wassira alianza kuzungumza nae kwa kile kilichoelezwa kuwa akubali kuiunga mkono bajeti hiyo.
Mpina alipotafutwa kuzungumzia hatua yake ya kutopiga kura alisema, Lukuvi alimwendea na kumweleza kuwa kwa sababu Muswada wa Sheria ya Fedha utajadiliwa baada ya bajeti kumalizika kuna nafasi ya kuzitafuta fedha hizo kwenye bajeti za wizara.
Alisema pamoja na maelezo ya Waziri Lukuvi alishindwa kuingia na kupiga kura kwa maelezo kuwa Dk. Mgimwa wakati akihitimisha hotuba ya bajeti hakujibu hoja zake kama alivyoelezwa na Lukuvi.
Alisema bado kuna nafasi nyingine ambapo atatoa hoja zake kwenye bajeti za wizara zinazofuata na mwishowe kwenye huo Muswada wa Sheria ya Fedha.
“Sikuweza kupiga kura kwa sababu sikuelewa kama hoja zangu kweli zimezingatiwa…maana yake niseme “ndiyo” kwa nini na nisema “hapana” kwa nini wakati hoja zangu hazijajibiwa,” alisema.
Wabunge walionekana kupiga makofi wakati majina ya wabunge ambao awali walionyesha msimamo wa kupinga bajeti hiyo walipopiga kura za ndiyo au hapana.
Mapema siku moja kabla ya kupitisha bajeti hiyo, juzi usiku, baadhi ya mawaziri na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walikesha kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuweza kupangua hoja zilizotolewa na wabunge kuhusiana na bajeti hiyo.
Chanzo cha habari hizi kimesema kuwa kikao hicho ambacho kilianza saa 3.30 usiku na kumalizika saa 9.30 alfajiri, kilifanyika chini ya Waziri Mkuu Pinda.
Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa kikao hicho kilifanyika nyumbani kwa Waziri Mkuu eneo la Uzunguni mjini hapa.
Baadhi ya mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Dk. Mgimwa, Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu na Waziri Lukuvi.

Idadi ya kura zilizopigwa na kusema ndiyo ni 225 na kura 72 zilisema hapana wakati wabunge 54 hawakuwepo.
Mapema akitoa majumuisho ya michango ya wabunge kuhusu bajeti ya serikali, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Mgimwa, alisema Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa  viwanda vya nguo, lakini haikupunguza kodi ya pato la mishahara kwa (PAYE) inayotozwa kwa wafanyakazi.
Kadhalika, alitangaza kuanzia mwaka huu wa fedha wafanyabiashara wanaopata faida ya shilingi milioni tatu kwa mwaka hawatalipa kodi ya mapato badala yake kodi hiyo itaanza kutozwa kwa  wafanyabiashara wanaopata faida  inayoanzia shilingi milioni nne kwa mwaka.
Kwa mujibu wa maelezo hayo wafanyabiashara wa ‘boda boda’ wamefutiwa kodi ya mapato.
Aidha alisema serikali imekubali kuondoa  VAT kwa  viwanda vya mafuta ya kula  lakini pendekezo hilo litawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki kwa maamuzi zaidi na maelekezo yake yataletwa wakati wa mjadala wa muswada wa fedha.
Kadhalika alisema serikali haitaweza kuongeza kima cha mshahara kufikia  Sh. 315,000 kwa mwezi kwani kutaongeza bajeti ya uendeshaji kwa kiasi cha Shilingi trilioni sita.
Akijibu hoja ya wabunge kutaka kujua maeneo yaliyosababisha deni la taifa kukua kutoka trilioni 5 mwaka 2009 hadi kufikia trilioni 20 mwaka wa fedha wa 2012/13 alisema, miradi iliyosababisha deni hilo kukua ni pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Mkula hadi Kigoma.
Nyingine ni barabara za Dar es Salaam – Somanga,  na Shelui -Nzega, Singida –Babati—Minjingu.
Pia mradi wa umeme wa Songosongo, Kihansi, mradi wa umeme wa Nyakato  na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria  na ukarabati na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Songwe na  Mwanza.
Jumla ya Sh. trilioni 15, zilipitishwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo na kuendesha shughuli za serikali kwa mwaka 2012/13.
Imeandikwa na Gaudensia Mngumi, Sharon Sauwa na John Ngunge, Dodoma.



CHANZO: NIPASHE

No comments: