ASEMA FIGO ZAKE ZIMESHINDWA KAZI, ZATAKIWA DOLA 40,000 KUMPELEKA INDIA
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
imebadilika na kuwa mbaya, baada ya figo zake kushindwa kufanya kazi ya
kuchuja sumu ya mwili na kusababisha apatiwe huduma ya kusafisha damu
yake.Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na kiongozi wa jopo la madaktari wanaoendelea kumtibu, Profesa Joseph Kahamba, zilieleza kuwa hali ya Dk Ulimboka ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo kuwapo mikakati wa madaktari wenzake kukusanya fedha ili kumpeleka nje ya nchi.
Dk Ulimboka ambaye amelazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alipatiwa huduma hiyo jana asubuhi kwa kutumia mashine maalumu, iliyoko katika Kitengo cha Watoto cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Daktari huyo ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, amelazwa kutokana na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha, meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano.
Tangu alazwe MOI baada ya kuokotwa na wasamalia wema, katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dares Salaam, hali ya afya ya Dk Ulimboka imekuwa tete na jana ilizidi kuwa mbaya.
No comments:
Post a Comment