MADAKTARI 146 wamefukuzwa katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na
kushiriki mgomo unaoendelea nchi nzima kwa lengo la kuishinikiza
Serikali kutekeleza madai yao.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini
kuwa, madaktari hao walitimuliwa katika Hospitali za Bugando na Sekou
Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ile ya
Rufaa Dodoma.
Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, mgomo huo
jana uliendelea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ocean Road,
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) za jijini Dar es Salaam, Hospitali ya
Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Katika
kile kinachoonekana kuwaunga mkono wenzao, madaktari bingwa wa MOI, MNH
na Ocean Road jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuingia
kwenye mgomo huo hadi madai hayo yatekelezwe.
Madai ya madaktari
ni hali bora ya mazingira ya utoaji huduma nchini, ongezeko la
mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za
kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.
Tamko
la madaktari hao bingwa, lilitolewa jana na msemaji wao, Dk Catherine
Mng'ong'o muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichofanyika
jijini Dar es Salaam.
Tamko hilo limekuja siku moja baada ya
baadhi yao kuanza kushiriki mgomo huo juzi, kushinikiza pamoja na mambo
mengine, Serikali itoe tamko juu ya tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa
Dk Ulimboka.
Hata hivyo, wakati madaktari hao wakitoa tamko hilo,
uongozi wa Moi jana ulitoa tangazo kuwataka madaktari wote walioshiriki
mgomo huo kurejea kazini ifikapo Julai 2, mwaka huu, vinginevyo
watafukuzwa kazi.
Jana jengo la MOI lilikuwa limefungwa kwa
makufuli, huku wagonjwa wakielezwa kuwa huduma zote hazitolewi zikiwamo
za dharura ambazo awali ziliendelea kutolewa.
Mmoja wa walinzi aliwambia waandishi wa habari kuwa, amefunga mageti kutokana na amri ya mkuu wake wa kazi.
“Mimi
ninatekeleza amri ya bosi wangu, amenitaka kufunga geti na hakuna mtu
kuingia, awe mgonjwa au ninyi waandishi wa habari kwa kuwa hakuna huduma
zinazotolewa humu,” alisema.
Mkoani Mwanza
Madaktari 63 walio
katika mafunzo ya vitendo kazini wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando,
Hospitali ya Mkoa Sekou Toure wametimuliwa na kurejeshwa wizarani
kutokana na mgomo huo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Dk Charles Majinge alisema kuwa, juzi aliwataka madaktari
waliokuwa katika mgomo kurejea kazini, lakini hawakufanya hivyo na jana
akaamua kuwarejesha 47 wizarani.
Katika Hospitali hiyo ya Mkoa wa
Mwanza Sekou Toure, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Valentino Bangi alisema,
madaktari 16 wamesimamishwa kufanya kazi kutokana na agizo la wizara.
No comments:
Post a Comment