Na Luqman Maloto
Katika mfano wa Shadrack na Shania, wiki iliyopita tulikomea kwenye sehemu inayosema: Usiku mmoja akiwa amelala, Shadrack alikurupushwa na mlio wa SMS, aliposoma kumbe ilitoka kwa Shania akimtaarifu kwamba siku iliyofuata ndiyo ndoa yake.
Shadrack alichanganyikiwa, akaja kugundua kwamba kumbe muda wote Shania alikuwa na mchumba lakini akawa anamdanganya.
Kilichomuumiza zaidi Shadrack ni jinsi mrembo huyo alivyomuandikia maneno mafupi. Kwani Shania wala hakuonesha kuguswa, hata kuomba msamaha japo wa kinafiki kwa kumpotezea mwenzake muda, hakufanya hivyo. Aliandika: “Tomorrow is my wedding.”
Usiku mzima Shadrack hakulala, maneno: “Tomorrow is my wedding,” yalijirudia kichwani na kuzidi kumuumiza. Alijiona mwanaume bwege kuliko maelezo. Maisha yake ya kimapenzi aliyaona yamejaa mikosi. Kila siku wa kutendwa ni yeye, tena anayemtenda ni mwanamke huyohuyo.
Siku iliyofuata alifanya kazi zake kwa kujivuta, hakuwa mzuri kiutendaji. Alishindwa kutekeleza mambo muhimu kwa ajili ya maisha yake. Muda wote alimfikiria Shania, kuna wakati alitamani kwenda kufanya fujo harusini lakini mwisho aliamua kuyaacha yapite. Akapiga moyo konde.
Akasahau machungu taratibu na akamudu kutojionesha mbele za watu ana machungu moyoni kwa sababu hata alipokuwa na Shania, alishajua kwamba ni mtu anayejali zaidi fedha kuliko mapenzi na utu.
Japo alijiona yeye ni fungu la kukosa, taratibu akaacha kujitoa kasoro na kujiamini yeye ni mwanaume sahihi, ila mwanamke wake ndiye alikuwa mapepe.
Shadrack alianza uhusiano na mwanamke mwingine. Mwanzoni ilimsumbua, kwani alihisi naye atamtenda kama yule wa mwanzo. Hata hivyo, akawa mwangalifu zaidi, baada ya muda, akabaini kwamba huyo ni mwanamke anayeweza kukidhi mahitaji yake ya kimaisha, kwa hiyo akafunga naye ndoa.
Maisha ya Shadrack yakawa mazuri, mambo yakamnyookea zaidi. Wakati upande wa pili, Shania hali ikawa siyo ile aliyoitarajia. Kumbe mwanaume aliyemuoa, ni mume wa mtu na hata hali ya kimaisha aliyokuwa anaoneshwa kabla, ilikuwa ni kiini macho. Kimsingi, mwanaume huyo alimkaanga kwelikweli.
Wakati Shania anaolewa, alifuta namba za simu za Shadrack. Alionesha wazi kwamba hamtaki tena, kwa maana alimpata mtu wa kutimiza matarajio yake ya kimaisha. Miezi saba baada ya ndoa, hakukuwa na mawasiliano kati yao. Kumbe, Shania alikuwa kwenye mateso kwa takriban miezi mitano.
Mpaka wakati huo, Shania aliweza kufurahia ndoa kwa miezi miwili tu. Baada ya hapo ilikuwa ni mateso makubwa, kwani aliweza kubaini kwamba mume wake ni mume wa mwanamke mwingine. Shania akawa mtu wa vilio kila kukicha. Ikabidi aende mahakamani kudai talaka.
Akakumbuka mbachao. Shadrack ndiye mbachao chake. Namba za simu hana, akatafuta marafiki wa Shadrack, wakampa namba za simu, kuanzia hapo ikawa usumbufu. Alipiga simu kila baada ya dakika tano, akitaka apokelewe tena, kwani amejifunza mengi, eti anaamini Mungu alimuadhibu kwa makosa aliyomtendea.
“Naamini wewe ndiye mwanaume wa maisha yangu Shadrack, naomba unipokee mwenzio,” Shania aliandika SMS za namna hiyo nyingi sana. Alipojibiwa kwamba haiwezekani, kwani ameshaoa mwanamke mwingine, Shania alisisitiza kwamba hata kuwa mke wa pili kwa Shadrack inawezekana.
Shadrack akamuuliza, kama yupo radhi kuwa mke wa pili, ni kwa nini asikubali kwa mume wake wa sasa? Shania akajibu: “Huyu mwanaume ni tapeli, kwako nipo tayari kuwa mke wa pili, hata kuwa nyumba ndogo bila ndoa. Naamini ulioa mwanamke mwingine kwa ujinga wangu.”
Shania alihangaika sana lakini mwisho Shadrack alifunga milango. Leo hii Shania alishafanikiwa kupata talaka yake kutoka mahakamani, anaishi kwa mateso. Aliyedhani ni mwanaume bora, kumbe ni tapeli na aliporudi kwa Shadrack kwa kudhani ni atakuta nafasi ipo, akakuta pamejaa.
Akatimiza lile angalizo langu kwamba angalia makini ulipo, unaporukaruka, utajikuta umepoteza almasi, wakati ulipokuwa bize kukusanya mawe. Hii ina maana kuwa unapaswa kuwa makini kila hatua ya maisha yako. Mapenzi ni fursa, mara nyingi haiji mara mbili.
Ni kwa nini uruhusu kujuta baadaye? Tamaa zako haziwezi kukidhi matarajio yako ya kimaisha, kwani unaweza kupata kama ya Shania. Vilevile, lipo kundi kubwa la wanaume ambao leo hii wanateseka, kwa sababu waliwachezea wanawake wa maisha yao, wakavamia magubegube, leo hii ni mateso mtindo mmoja.
www.globalpublishers.info
1 comment:
Kwa upande mmoja hii inanihusu na mimi pia. 'Maana unakumbuka shuka kumekucha'
Post a Comment