ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, June 30, 2012
Simba yatupwa kundi la kifo Kagame
Sosthenes Nyoni
MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame Yanga wamepangwa kundi mchekea, huku mahasimu wao Simba wakitupwa kundi la kifo katika mashindano hayo yatakayoanza kupigwa Julai 14 jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo ambayo kwa mwaka wa tatu mfululizo yanafanyika katika ardhi ya Tanzania yatashirikisha timu 11 ikiwamo APR (Rwanda),Wau Salaam (Sudan Kusini), Atletico (Burundi), Simba, Yanga, Azam (Tanzania), Tusker(Kenya), Ports (Eritrea), URA (Uganda) na Vital Club ya Congo DRC.
Ikitokea kundi C, Yanga itafungua pazia la mashindano hayo kwa kuwakabili mabingwa wa Burundi timu ya Atletico katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 8 mchana kabla ya baadaye jioni kushuhudiwa mechi nyingine za kundi hilo kati ya Wau Salaam ya Sudan Kusini na APR ya Rwanda.
Kwa upande mwingine, Simba iliyoswekwa kundi A itasubiri hadi Julai 16 pale itakapokwaana na mabingwa wa Uganda timu ya URA katika pambao litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Vigogo wengine wanaokamilisha kundi C mbali ya Simba na URA ni Vital Club ya Burundi na mabingwa wa Djibout,Ports.
Kwa mujibu wa Ratiba ya Mashindano iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Azam FC wamepangwa kundi B pamoja na timu za Mafunzo na Tusker ya Kenya.
Azam FC ambayo itashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza, itaanza kampeni yake Julai 15 kwa kukwaruzana na Mafunzo katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi Complex nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Timu nane zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati kundi B litatoa timu mbili.
Katika hatua nyingine, Musonye alisema timu za El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu kutokana na sababu tofauti.
Akifafanua zaidi, Musonye alisema Coffee imeshindwa kushiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14, wakati El Merreikh inakabiliwa na mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Alisema Cecafa imeiondoa Red Sea kutokana historia ya wachezaji wa timu hiyo kutokomea kusikojulikana baada ya kuondolewa mashindanoni na kudai kwamba ukosefu wa amani nchini Somalia kama sababu za Elman kutoshiriki.
Bingwa wa mashindano hayo atapata dola 30,000, wakati mshindi wa pili atapata Dola 20,000 huku yule wa tatu ataondoka na dola 10,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment