Akizungumza na NIPASHE Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Charles Kenyela, alisema juzi jeshi hilo lilishindwa kuwahoji walinzi hao kutokana na hali zao kuwa mbaya na kushindwa kuongea vizuri.
“Tulipata ugumu wa kuwahoji kutokana na hali yao kuwa mbaya, lakini hivi sasa ndiyo wametolewa katika hospitali ya Mwananyamala walikokuwa wamelazwa, wanapelekwa kituoni kwa mahojiano,” alisema.
Kuhusu mali zilizoibwa, Kenyela alisema wamefanikiwa kupata funguo za magari, televisheni moja aina ya Sumsung, nyaraka na hundi za benki.
Aidha, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Ernest Mchome, alisema japo wanasikitika kwa tukio hilo, hakuna tatizo juu ya upotevu wa kumbukumbu na taarifa mbalimbali kwa sababu zimehifadhiwa katika mfumo wa kiteknolojia.
“Tumepotelewa na vitu mbalimbali, lakini tunashukuru Mungu tuligundua mapema tukatengeneza mfumo maalum wa kuhifadhi taarifa kwa mtindo wa kiteknolojia, kwa hiyo taarifa zetu zimehifadhiwa angani,” alisema.
Juzi watu wanaodaiwa kuwa wezi walivamia ofisi za TCU na kuwalewesha walinzi chakula kinachodaiwa kuwa na dawa za kulevya na kisha kuvunja na kupora fedha, nyaraka na mali mbalimbali.
Wakati huo huo Kenyela alisema, tayari jeshi la Polisi Kinondoni limepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali fuvu la kichwa kilichokutwa katika baa inayojulikana kama Bongo Star inayomilikiwa na James Isame mkazi wa Kawe, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Aidha aliongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa mara baada ya kumalizika kwa uchunguzi na kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment