ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 27, 2012

Wawakilishi watikisa Muungano


Mjadala mkubwa umeibuka kuhusu maslahi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huku Wajumbe wa CUF wakitamka wazi kuwa hawautaki.

Mjadala huo ulijitokeza jana ndani ya Baraza la Wawakilishi (BLW), wakati wakichangia Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili katika kikao cha Bajeti kinachoendelea, Chukwani Zanzibar jana.

Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF), Salehe Nassor Juma, alisema yeye hataki Muungano kwa vile Zanzibar imekuwa hainufaki kiuchumi kutokana na mfumo wa sasa wa Muungano huo.

“Mimi niseme wazi sitaki Muungano na katika kitu ambacho nakichukia sana basi ni huu muungano maana kwa miaka 48 kila siku tunaambiwa kuna kero wala hazitatuliwi basi ni uvunjike,” alisema.

Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM), Makame Mshimba Mbarouk, alisema mfumo wa sasa wa Muungano unainyonya Zanzibar na kutoa mfano kwamba visiwa hivyo havinufaiki na gesi asilia tangu kuanza kuvunwa Tanzania Bara.

“Lazima Wazanzibari tuamke muungano huu, siyo...tunaotaka na tunataka haki zetu zote kuanzia mapato ya gesi, nitazuia bajeti hii mpaka niambiwe Zanzibar imepata kiasi gani kwa mapato yanayotokana na gesi tangu kuanza kuvunwa Tanzania Bara,” alisema Mshimba.



Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chonga (CUF), Abdalla Juma Abdalla, aliwataka viongozi wa serikali kuacha kubeza maoni ya wananchi wanaopinga mfumo wa sasa wa muungano.

“Kiongozi yeyote kuanzia Rais, wabunge, hata sisi wawakilishi tumewekwa hapa kwa kuchaguliwa na wananchi na kazi yetu kubwa kusimamia serikali na kutetea maslahi ya wananchi wetu,” alisema.

Alisema iwapo wananchi wa jimbo lake watasema hawataki Muungano atasimama nao bega kwa bega kutetea hoja yao kwa sababu wamemchagua kwa kumuamini na bado anahitaji kurudi tena katika chombo cha kutunga sheria.

Asha Bakari Makame (Viti Maalum CCM) na makamu Mwenyekiti wa UWT, alisema Wajumbe wa Baraza hilo wanajukumu kubwa la kutetea maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.

Alisema wakati umefika kwa Wawakilishi kurejesha imani kwa wananchi kwa kuhakikisha maslahi ya Zanzibar na wananchi wake yanalindwa na kutetewa ndani ya Muungano huo.

Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lazima iwe makini na kuacha tabia ya kuridhia kila jambo linaloanzishwa na Serikali ya Muungano.

Alisema kwamba matatizo ya kero za Muungano yamekuwa yakichochewa na viongozi kutokana na kushindwa kuzitatua.

Awali, akiwasilisha Makadirio na Matumizi ya bajeti yake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta faida kubwa za kiuchumi na kiusalama kwa wananchi wa pande zote.
CHANZO: NIPASHE

No comments: