ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 9, 2012

DR. ASHA-ROSE MIGIRO KUWASILI LEO ALASIRI, VIONGOZI WA UN TANZANIA KUMPOKEA AIRPORT.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyemaliza muda wake Dr. Asha-Rose Migiro anawasili leo na ndege ya Emirates na atapokelewa na viongozi wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa waliopo Tanzania, wakiongozwa na Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Dkt. Alberic Kacou.


Wakati Dk. Asha-Rose Migiro, anarejea leo nchini baada ya kumaliza muhula wake katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), amesema nafasi hiyo imempatia uzoefu mkubwa katika nyanja mbalimbali za kimataifa.


Akitoa tafakuri yake juu ya muhula wake katika nafasi hiyo, uliodumu kwa miaka mitano na nusu, Dk. Mingiro amemshukuru Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon, kwa kumpa fursa hiyo, Rais Jakaya Kikwete na Watanzania kwa kumpa moyo na kumuenzi wakati wa utumishi wake.

Dk. Migiro alisema kwa kufanya kazi na UN, amepata fursa ya kuchangia juhudi za pamoja za kuimarisha umoja huo kutekeleza majukumu yake katika kipindi kigumu kimataifa na chenye changamoto nyingi.

“Utumishi wangu katika Umoja wa Mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia, kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia,…na changamoto nyingine nyingi,” alisema.

Hata hivyo, Dk. Migiro alisema wakati akimaliza muhula wake, anatiwa moyo na taarifa kuwa juhudi za kupambana na umaskini duniani zimeanza kuzaa matunda licha ya ukweli kuwa dunia kwa sasa inapita katika kipindi kigumu kiuchum kuliko wakati mwingine wowote kwa miaka ya karibuni.

Katika tafakuri yake, Dk. Migiro alizungumzia mafanikio pia changamoto kwenye nyanja mbalimbali ambazo yeye na watumishi wenzake kwenye taasisi hiyo ya juu kimataifa wameyafanyia kazi.

Baadhi ya maeneo aliyoyazungumzia ni pamoja na Malengo ya Maendeleo ya Milenia barani Afrika, mkutano wa Rio + 20, usawa wa kijinsia, afya ya jamii, mageuzi katika menejimenti ya UN na utawala wa sheria.

Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa, Dk. Migiro alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Rais Jakaya Kikwete.

No comments: