ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 16, 2012

Mjane wa Karume aichana Serikali


Mwandishi Wetu
WAKATI taifa likiwa katika mchakato wa kuelekea kupata Katiba Mpya, Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume ameibuka na kusema kama mumewe (marehemu Abeid Aman Karume) angekuwapo, baadhi ya mambo yanayofanywa na Serikali kuhusu Muungano sasa asingeyakubali.
Akizungumza katika mahojiano maalumu katika Kipindi cha Kutoka Zanzibar kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Channel Ten, mwishoni mwa wiki Mama Karume alisema kuwa, Muungano una kero nyingi ambazo sasa zinauingiza katika matatizo.

Alisema kero hizo hata mumewe marehemu Abeid Aman Karume angekuwa hai, asingezikubali.

Mama Karume, ambaye alijinasibu kama muumini mkubwa wa Muungano, alisema mumewe hakuiunganisha Zanzibar ili imezwe bali, alitaka nchi zote mbili za Muungano ziunganishwe na kunufaika kwa usawa.
"Mzee Karume alikubali Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuwa aliamini, kutatokea taifa moja lenye nguvu," alifafanua Mama Karume na kuongeza:
"Alijifunza kutoka Marekani ambayo ni Muungano wa majimbo mengi na iliyokuwa Muungano wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Sovieti (USSR). Alijua Tanzania nayo itakuwa na nguvu za kisiasa na kiuchumi."

Mama Karume pia alifahamisha kuwa alikutana na viongozi wa Kundi la Uamsho lililoko Zanzibar na kuwasikiliza na kusema kuwa, anaunga mkono madai yao.
Hivi karibuni Kundi la Uamsho lilisababisha kuzuka kwa vurugu zilizoambatana na  kuchoma makanisa na kuongoza mijadala mikali ya kupinga Muungano, kiasi cha kufanya baadhi ya viongozi wake kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

"Unajua vijana wa siku hizi wanajua mengi yanayoendelea kwenye Muungano. Kwa sasa na kwa kweli napenda kusema hawa watu wa Uamsho walinifuata nyumbani na wakanieleza kero zao kuhusiana na Muungano kwa kweli wana hoja," alisema na kuongeza:

"Mimi naupenda sana Muungano lakini, kwa sasa nadhani una matatizo mengi, ambayo yanapaswa kujadiliwa kwa ukweli na uwazi. Nadhani hawa watu wa Uamsho wasikilizwe," alisema Mama Karume, ambaye mumewe aliuawa Aprili 7, 1972 katika eneo la Kisiwandui Zanzibar.
Uteuzi wa watendaji Muungano
Pia Mama Karume alisema kuwa, uteuzi wa viongozi wa taasisi ambazo zinatakiwa kuwa za Muungano una walakini akisema; katika na uteuzi wa mabalozi, Zanzibar ina mabalozi watatu kati ya 33 wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.
Pia alisema uongozi wa juu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tangu ianzishwe mwaka 1966, hasa Gavana hajawahi teuliwa kutoka Zanzibar.
Alikiri kuwa kuna Naibu Gavana kutoka Zanzibar, lakini alidai chini yake amewekewa watu wawili kutoka Bara. Naibu Gavana, ambaye anatoka Zanzibar anaitwa Juma Reli (Anahusika na Utawala).
"Hivi ni haki kweli Zanzibar kuwa na mabalozi watatu wa Tanzania au kuwa na Naibu Gavana aliyewekewa wasaidizi wawili? Nadhani kuna tatizo hapa. Haya mambo lazima yaongelewe," alisema mama  Karume.
Alisema hakubaliani na jinsi suala zima la usimamizi wa fedha linavyosimamiwa na Serikali ya Muungano.
Alisisitiza hata mume wake, Karume angekuwa hai mambo hayo asingekubaliana nayo, kwani tangu mwanzo alikuwa anavutana na Muasisi mwenzake Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
"Unajua, Mzee Karume alipokuwa hai alikuwa hataki masuala ya fedha na sarafu kuwa ya Muungano. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kumtuma Waziri wake wa Fedha, Amir Jamal kuja Zanzibar na alikataa kutoa fedha za Zanzibar kwenda Benki Kuu," alisema mama Karume.
Aliongeza; "Baada ya kitendo kile cha kumkatalia Jamal, nilimuuliza Mzee Karume inakuwaje anakataa kutoa fedha zile... Aliniambia kuwa kinachozalishwa Zanzibar kitabakia kuwa cha huku kwani haiwezekani kwa kisiwa kulisha nchi kubwa ya Tanganyika".
Adai katelekezwa
Katika hatua nyingine, Mama Karume alidai kuwa pamoja na kuwa mke wa mwasisi wa Muungano lakini, bado hajanufaika nao.
Mama Karume alilalamika kuwa, ametelekezwa na Serikali ya Muungano licha ya ukweli kwamba, mumewe alifariki akiwa Makamu wa  Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Alilalamika kwamba hajahudumiwa chochote na Serikali ya Muungano tangu mumewe afariki bali amekuwa akihudumiwa na Serikali ya Zanzibar na ndugu zake wa karibu.
"Hawa watu wa Serikali ya Muungano walinitelekeza maana hawajanisaidia chochote tangu Mzee Karume afariki.
“Kinachonishangaza ni wake za Makamu wa Rais wa Muungano waliofuata baada ya Mzee Karume wanaangaliwa na hata kupelekwa nje kwa matibabu," alisema na kuongeza;
"Ninaendesha maisha yangu vizuri, lakini kwa kweli sijasaidiwa na lolote na Serikali ya Muungano pamoja na ukweli kuwa mume wangu ni mwanzilishi wa Muungano huu."
Mtikisiko wa Muungano
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika siku za karibuni, umekuwa ukipita katika kipindi kigumu huku wanasiasa, wanaharakati na wananchi wakihoji muundo wake.
Wafuasi wa Kundi la Uamsho liliko Zanzibar walikamatwa hivi karibuni, wakihusishwa na uchomaji makanisa na uendeshaji wa mijadala ya kuelezea kero za Muungano.
Hata hivyo, malalamiko hayajaanza leo kwani yamekuwako miaka na miaka kiasi cha kufanya mwaka 1984, Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, Waziri Kiongozi  Ramadhan Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Swanzey kulazimishwa kujiuzulu katika kile kilichoitwa kuchafuka kwa hali ya hewa huko Zanzibar.

Tayari suala hilo la Muungano limeanza kuibua mjadala visiwani Zanzibar katika mchakato wa kupokea maoni unaofanywa na Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.

Mwananchi

3 comments:

Anonymous said...

mmeona mambo na unaona ukiwa ukweli uko uongo hujitenga si mlisema kikundi cha UAMSHO NI CHA WANUNI sasa mama karume anaweza akawasikiliza wahuni hawa na kukubalia nao.
na makanisa wala hayajachomwa ni fix tu kutaka kukichafua kikundi hichi lakini njama zao this time zimegonga ukutaa.
na yaleyochomwa moto haya makanisa yalikuwa si makanisa nasema hivi kwa sababu ushahidi ninao walikuwa hawajapata kibali cha kumiliki sehemu ile na ilikuwa si sehemu ya ibada kulivyotokea machafuko ndo wakaenda mbio juu chini kutafuta kibali cha kumiliki sehemu hizo

kila siku mtu utasema uongo utawadanganya watu na kuwazulumu haki yao lakini daima katu abadan haki ya mtu hachukuliki wala haliki na ukweli daima utadhihiri

uamsho daima na tunataka nchi yetu na hatutasinzia au kulala usingizi wa pono mpaka kieleweke.ZANZIBAR YETU HURU tunaitaka

dj luke shukran sana mkuu kwa kutuwekea kitu hichi poa maridhawa umenikosha nafsi yangu kwa siku ya leo

mdau New York

Anonymous said...

Mimi sioni sababu ya sisi watanganyika kuendelea kuwang'ang'ania hawa jamaa wa zanzibar...kwanza kabisa sisi hatuna kitu chochote tunachopata toka huko na wala hatuwezi kudhurika na kitu chochote kama muungano ukiwa..Hiyo zanzibar ni broke,hakuna dili yoyote kule mimi nimekaa miaka mitatu kule...tuwaache waende
madau kansas city,Mo.

Anonymous said...

Mdau wa Kansas City, MO - unaonekana huijuwi historia ya Zanzibar kiasi useme hivyo kwamba hakuna dili ni broke. Zanzibar imefanywa kuwa vile kwa makusudi na Tanganyika na kusaidiwa na Waingereza ili kuidhoofisha kwa udanganyifu wa Muungano. Njia zote kuu za uchumi zimehamishwa Tanganyika na hakuna kimoja kinachofanywa baada ya uzembe na ubadhirifu, kila siku zikienda umaskini unazidi kwa dhulma. Kasome historia ya Zanzibar kiuchumi ilikuwa wapi kabla ya Muungano halafu ndio uzungumze kuhusu Zanzibar.
Mdau California.