ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 18, 2012

Yanga yawachakaza vibonde Wau


Beki wa Yanga, Stephano Mwasika akifunga bao la tatu mbele ya kipa wa El-Salam Wau ya Sudan Kusini akiruka bila mafanikio, katika mechi ya kuwania Kombe la Kagame, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda 7-1.Picha na Michael Matemanga
Sosthenes Nyoni
MABINGWA watetezi, Yanga waliwachakaza kwa mabao 7- 1 vibonde Wau Salaam wa Sudan Kusini katika mchezo wa michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Karamu hiyo ya Yanga iliongozwa na mshambuliaji Hamis Kiiza aliyefunga mabao matatu na Said Bahanuzi mawili,  huku Stephan Mwasika, Nizar Khalfan wakifunga bao moja kila mmoja, kabla ya Wau Salaam kupata bao la kufutia machozi dakika ya 90 kupitia kwa mshambuliaji wao Khamis Deshama.
  
Kwa ushindi huo Yanga bado imebaki nafasi ya tatu na pointi zake tatu baada ya mabingwa mara tatu APR ya Rwanda kulazimishwa suluhu na Atletico ya Burundi na kufikisha pointi nne kila moja, huku Wau Salaam ikishika mkia na rekodi ya kufungwa mabao 14 katika mechi mbili.

Katika mchezo huo kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake katika mechi ya jana kwa kuwaanzisha Bahanuzi mbele, Mwasika, Godfrey Taita na Khalfan badala yaJerryson Tegete, Rashid Gumbo, Shamte Ally na Godfrey Taita. Taita aliziba pengo la beki  Abdul Juma anayeuguza jeraha la kifundo cha mguu.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija  kwa Yanga,  ambapo Khalfan alianzisha mashambulizi kutokea upande wa kulia huku Haruna Niyonzima akicheza kama kiungo mshambuliaji.

Mshambuliaji Kiiza alikosa bao dakika ya 10 akiwa yeye na kipa wa Wau, Nizir Riham Taban  baada ya kupiga shuti dhaifu, lakini dakika mbili baadaye Bahanuzi alifunga bao la kwanza akiunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Niyonzima.

Yanga iliyokuwa ikitumia mfumo wa 4-3-3 ilionekana kuwazidi ujanja Wau Salaam waliocheza 4-4-2 kwani dakika 17, Kiiza alipitisha pasi nzuri iliyotua mguu kwa Bahanuzi aliyepiga shuti kali na kujaa wavuni na kuipa Yanga bao la pili.

Washambuliaji wa Yanga walioshutumiwa kwa kukosa umakini kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Atletico jana walikuwa tofauti kabisa kwani Kiiza aliyekuwa nyota wa mchezo alifunga bao la tatu kwa mabingwa hao dakika ya19 kwa kuwapora mpira mabeki wa Wau na kuutumbukiza mpira wavuni.

Mwasika aliwainua mashabiki wachache wa Yanga waliokuwa uwanjani hapo kwa kufunga bao la nne kwa kumpiga kanzu kipa Taban na kuingia wavuni katika dakika ya 25. 

Kiiza alifunga bao lake la pili dakika ya 30 likiwa ni bao la tano kwa Yanga baada ya kuunganisha kwa kisigino krosi iliyopigwa na Bahanuzi aliyekuwa mwimba kwa ngome ya Wau na dakika tano baadaye Kiiza aliifungia Yanga bao la sita.

Katika mchezo huo Wau walicheza bila ya maelewano na walikuwa wakipoteza pasi nyingi ila mchezaji mmoja mmoja katika timu hiyo walikuwa na uwezo wa juu.

Kocha wa Yanga katika mechi hiyo alimtoa Kelvin Yondani na kumwingiza Juma Seif na kumlazimisha Athuman Idd kurudi kucheza namba nne kabla ya kumpumzisha Niyonzima na kumwingiza Rashid Gumbo dakika ya 53.

Yanga iliendelea kulisakama lango la Wasudani hao na dakika ya 66, Khalfan aliwatoka mabeki wa Wau na kupiga shuti nje akiwa yeye na kipa, lakini dakika tatu baadaye Kiiza alifunga bao akiunganisha krosi ya Nizar, lakini mwamuzi Issa Kagabo alilikataa kwa madai mfungaji ameotea.

Kiungo wa zamani wa Vancover Whitecaps, Nizar aliifungia Yanga bao la saba dakika ya 75 akimalizia pasi ya Kiiza, kabla ya Wau kupata bao la kufutia machozi kupitia Deshama aliyefunga kwa shuti la chini lililomshinda kipa Yaw Berko.

Akiuzungumzia mchezo huo kocha wa Wau, Sebit Bol aliishukuru Cecafa kwa kuwapa nafasi ya kushiriki michuano hiyo pamoja na vipigo imewasaidia kupata uzoefu.

"Hii ni mara yetu ya kwanza kushiriki michuano hii naamini tumejifunza mengi na kupata uzoefu wa kutosha,"alisema Bol.

Naye kocha wa Yanga, Seintfiet aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri, lakini alisema kuna na nafasi walizipata na walishindwa kuzitumia vizuri kwani walistahili kufunga mabao 10.

"Nawaza sasa mchezo wa mwisho dhidi ya APR,  nategemea kupata upinzani mkali kutoka kwa vigogo hao wa Rwanda kwa sababu ni timu pia nayoona ina uwezo wa kutwaa ubingwa wa mashindano haya,"alisema Saintfiet.


Mwananchi

No comments: