Wednesday, August 22, 2012

CEGODETA YAITAKA SERIKALI IFUNGE AKAUNTI ZA VIGOGO USWIS

TAASISI ya Utawala Bora na Maendeleo nchini (CEGODETA), imeiomba Serikali kuwasiliana na Serikali ya Uswisi ili kufunga akaunti za wanasiasa na wafanyabiashara wa Tanzania ambao wanadaiwa kutorosha na kuficha fedha zao nchini humo.


Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bw. Thomas Ngawaiya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema taasisi hiyo imefadhaishwa na taarifa ambazo zimetolewa na baadhi ya wabunge juu ya wanasiasa na wafanyabiashara ambao wametorosha na kuficha fedha hizo sh. trilioni 11.6.

"Fedha hizi zinakaribia bajeti ya Serikali kwa mwaka mzima, wabunge wamedai upo ushahidi wa madai yao kutokana na taarifa ambazo zimetolewa na Global Financial Integrity.

"Pia wanadai kupata taarifa za siri kutoka Benki Kuu ya Uswisi, ambayo imeonesha kuna dola za Marekani zipatazo 315 sawa na sh.bilioni 478 za kitanzania ambazo zimefichwa nchini humo," alisema.

Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa, kuna baadhi ya wanasiasa ambao hawana uchungu wala uzalendo bali kipaumbele chao ni kujitajirisha wao binafsi na familia zao.

"Hii ni sababu mojawapo inayoifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, licha ya kuwa na rasilimali nyingi, hadi sasa asilimia 60 ya Watanzania wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku na mlo mmoja tu,"alisema.

Bw. Ngawaiya alisema fedha hizo zikirejeshwa nchini zitumike kuboresha sekta za elimu na afya kama ilivyofanyika katika fedha za rada na kuongeza kuwa, wote ambao itabainika wamehusika na hujuma hiyo bila kujali nyadhifa zao, wafikishwe mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi ili iwe fundisho kwa wengine.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake