KIONGOZI wa madaktari, Dk Stephen Ulimboka amewataka watanzania wasiwe
na hofu na wasubiri siku maalum ambayo ataweka wazi ukweli wote kuhusu
namna alivyotekwa na kuteswa, pia hali yake ya kiafya kwa sasa.
Dk
Ulimboka ambaye amerejea nchini hivi karibuni kutoka Afrika Kusini
alikokuwa amepelekwa kwa ajili ya matibabu alisema jana kuwa hawezi
kuzungumza lolote kwa sasa na aachwe apumzike kwani ameugua na
ametengana na familia yake kwa muda mrefu, hivyo anahitaji muda wa kuwa
peke yake.
“Niacheni nipumzike kwa sasa. Wakati muafaka ukifika,
nitasema yote. Sitaacha kusema, muda muafaka ukiwadia nitayasema
yaliyonitokea na taratibu maalum zitaandaliwa ili nizungumze na
watanzania,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema hawezi kuzungumza bila
utaratibu maalum bali atazingatia taratibu zitakazoandaliwa na uongozi
wa Jumuiya ya Madaktari (MAT) ndipo ataueleza umma na kusema yaliyo
moyoni kuhusu kutekwa na kupigwa kwake.
“Haya mambo yatawekwa
hadharani lakini ni kwa utarartibu maalum, si kama hivi mnavyotaka
ninyi. Kila mtu ananiuliza halafu mnakwenda kuandika ya kwenu, naona hii
imekuwa kama biashara sasa,” alisema.
Aidha Dk Ulimboka
alivilaumu baadhi ya vyombo vya habari kwa kuandika habari ambazo si za
kweli kuhusu suala la kutekwa na kuteswa kwake na kusema kuwa wamekuwa
wakipotosha ukweli wa tukio lenyewe.
“Wengine wananipigia simu na
kunijulia hali, nikiwaambia basi wanaenda kuandika tofauti, kwa mfano
juzi wameandika kuwa nimeonekana nikipanda boti, jambo ambalo si la
kweli,” alisema.
Akizungumzia hilo, makamu wa rais wa MAT, Prinus
Saidia alisema Dk Ulimboka kwa sasa yupo mapumzikoni na atazungumza kwa
kina baada ya muda mfupi.
Alisema madaktari wamekubaliana kuwa Dk
Ulimboka aachwe apumzike baada ya kipindi kigumu cha muda mrefu lakini
atazungumza kwa undani wakati ambao utakubaliwa na jumuiya hiyo.
Wakati
huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki za Raia, Siasa na
Mwenendo wa Bunge, Marcossy Albanie amesema ataitisha mkutano wa
waandishi wa habari siku ya Jumatatu ambapo pamoja na mambo mengine
atazungumzia suala la kutekwa na kuteswa kwa Dk Ulimboka.
Albanie
hakutaka kuweka wazi ni nini hasa ambacho atakwenda kuzungumzia kuhusu
Dk Ulimboka bali alisisitiza kuwa taasisi yake itazungumzia suala hilo
la kutekwa na kipigo cha daktari huyo.
1 comment:
Mungu ni mwema, tunashkuru Mungu ni mzima na anaendelea vizuri, tunazidi kumuombea ulinzi wa Mungu.
Post a Comment