MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora, leo inatarajia kutoa hukumu ya kupinga
matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora,
yaliyompa ushindi mbunge wa sasa, Dkt.Peter Kafumu (CCM).
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa
kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Bw.Joseph Kashindye ambaye amepinga matokeo hayo.
Katika kesi
hiyo, washtakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo,
Bw.Protace Mgayane.
Shauri hilo lilianza kusikilizwa Machi 26, mwaka huu na Jaji Mery Nsimbo Shangali.
Akizungumza
na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya
ya Nzega, Bw.Silvester Kainda, alisema awali Mahakama Kuu Kanda ya
Tabora, ilipanga kutoa hukumu Agosti 20, mwaka huu, bahati mbaya ilikuwa
sikukuu hivyo itasomwa leo.
Kwa upande wake, Wakili wa
Mlalamikaji Profesa Abdallah Safari, alisema zaidi ya malalamiko 13
waliyawasilisha mahakamani hivyo wapo tayari kusikia uamuzi wowote ambao
utatolewa.
Dkt.Kafumu anawakilishwa na mawakili wawili ambao ni
Bw.Antony Kanyama na Bw. Kayaga Kamaliza ambapo miongoni mwa malalamiko
yaliyowasilishwa na Bw.Kashindye ni pamoja na Bw.Kafumu kutoa vitisho,
ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbuntu na kugawa mahindi.
No comments:
Post a Comment