MAANDALIZI ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti
26, mwaka huu yameingia dosari baada ya matukio kadhaa ya kukwamisha
kazi hiyo kujitokeza katika mikoa mbalimbali, ukiwamo Dar es Salaam
ambako zaidi ya makarani 800 wamegoma kula kiapo cha utii na kutunza
siri.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa mbali na makarani
hao, vipeperushi vyenye ujumbe wa kutaka watu wagomee Sensa vimesambazwa
mkoani Arusha, huku mkoani Tanga kukiwa na tukio la Sheikh mmoja kutiwa
mbaroni kwa kusambaza vipeperushi vya aina hiyo.
Mgomo wa makarani
Makarani
hao waligoma jana ikiwa ni siku yao ya mwisho ya mafunzo ya kazi ya
kuhesabu watu na makazi. Makarani hao kutoka vituo mbalimbali
kulikotolewa mafunzo hayo, walisema wameamua kugomea kiapo hicho
kutokana na fedha zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya kazi hiyo
kuchakachuliwa kinyume na makubaliano.
Baadhi ya vituo ambavyo
makarani wake wamegoma ni Shule ya Sekondari Makumbusho, Kambangwa,
Shule ya Msingi Zawadi na vituo kadhaa vilivyopo maeneo ya Buguruni na
Kawe.Baadhi ya makarani hao walionekana wakiwa katika makundi, muda
ambao walipaswa kuendelea na mafunzo yao kabla ya kula kiapo cha
kushiriki Sensa kwa uaminifu na ukamilifu.Baadhi ya makarani ambao
waliomba majina yao yasitajwe gazetini, walisema imekiuka makubaliano ya
awali.
“Serikali imesema imetenga Sh141 bilioni kwa ajili ya
Sensa. Sisi tayari tuliingia makubaliano nayo kwamba tunatakiwa kulipwa
Sh35,000 kwa siku, kwa muda wa siku saba jambo ambalo limegeuka na kuwa
kinyume.”
“Ukipiga mahesabu fedha ambazo tungetakiwa kulipwa kwa
siku hizo saba ni Sh245,000 lakini wao wamekuja hapa na kutupa Sh140,
000 tu. Hatuwezi kuendelea na kazi mpaka tulipwe fedha zetu.”
Karani
mmoja katika Kituo cha Sekondari ya Kambangwa, alisema wameamua kugomea
kiapo baada ya kuona kuwa mpaka mafunzo yanahitimishwa jana, baadhi yao
hawajalipwa chochote.
RC Dar:Watalipwa
Akizungumzia madai ya
makarani hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema
mpaka jana mchana makarani wote walipaswa kulipwa awamu ya pili ya fedha
zao. Alisema awamu ya kwanza ya malipo hayo ilifanywa katika siku tano
za mwanzo.“Kuna watu wamejichomeka katika zoezi hili, lakini kama kweli
karani ameteuliwa lazima atalipwa pesa zake na kama imetokea
amesahaulika basi afanye mawasiliano na mratibu wa Sensa wilaya
anayotoka ili alipwe,” alisema.
Sheikh mbaroni
Katika hatua
nyingine Sheikh Juma Koosa (52) anashikiliwa na polisi wilayani Morogoro
akituhumiwa kutumia kipaza sauti kuwatangazia wananchi wasishiriki
Sensa.
Sheikh huyo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa
Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, alikamatwa Agosti 19 mwaka huu
alipokuwa kwenye Msikiti wa Miembeni, Mazinde mara baada ya kukaribishwa
na wenyeji wake kuzungumza.Imedaiwa kuwa Koosa alitoa kitabu chenye
kueleza sababu za kuwakataza Waislamu kutokushiriki Sensa mwaka huu.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema Sheikh huyo pia
alikutwa na nakala 15 za kitabu hicho.Alisema alikamatwa kutokana na
taarifa za baadhi ya waumini ambao walichanganywa na taarifa za mgeni
huyo... “Baadhi ya waumini walikubaliana naye huku wengine wakimpinga.
Hivyo mtafaruku ukajitokeza na ndipo wale waliopinga wakawasiliana na
polisi ambao walifika na kumkamata.”
Baada ya kukamatwa alipelekwa
Kituo cha Polisi Mombo kwa mahojiano zaidi na kuhamishiwa Makao Makuu
ya Polisi Wilaya ya Korogwe, baada ya kuwapo kwa dalili za baadhi ya
waumini kuandamana kupinga hatua hiyo.Alisema, mtuhumiwa huyo
anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
CWT
Kaimu
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch amewataka
walimu kutosita kudai masilahi yao kwa kuhofia Serikali kuwaondoa
katika shughuli mbalimbali za kitaifa.
Oluoch alisema jana kwamba
wanao ushahidi wa maandishi kuwa kuondolewa kwa baadhi ya walimu katika
Sensa kumetokana na kushiriki kwao katika mgomo ulioandaliwa na CWT kwa
lengo la kudai masilahi yao sekta nzima ya elimu nchini.
Alisema
CWT bado ipo katika mchakato wa kukusanya takwimu kwa wanachama wake
waliotolewa katika Sensa nchi nzima na imebaini kuwa Serikali imefanya
hivyo kama njia ya kuwakomoa.
“Tumepata ushahidi unaoonyesha kuwa
walimu wamekatwa kwenye zoezi la Sensa kutokana na kushiriki mgomo”
alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo haitarudisha juhudi za walimu za
kudai masilahi yao kwani madai yao ni muhimu.
Habari hii imeandikwa na Mashaka Kibaya, Korogwe, Aidan Mhando, Fidelis Butahe na Elizabeth Edward
No comments:
Post a Comment