JESHI la Polisi Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, linamshikilia Shekhe
Juma Koosa (52), mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kutumia
kipaza sauti akiwa msikitini na kuwatangazia waumini wa Kiislamu
wasishiriki Sensa ya Watu na Makazi.
Shekhe Koosa ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa
pili katika Chuo Kikuu cha Kiislamu mkoani Morogoro, alikamatwa Agosti
19, mwaka huu katika Msikiti wa Miembeni, uliopo Mazinde baada ya
kukaribishwa na wenyeji wake.
Baada ya kukaribishwa na wenyeji
wake, Shekhe Koosa alieleza sababu za kuwataka Waislamu wasishiriki
sensa na kusoma ujumbe ulioandikwa na Bw.Matimba kupitia kitabu chake
chenye kurasa 31.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Bw.Constantine
Massawe, alithibitisha kukamatwa kwa Shekhe Koosa ambaye alikutwa na
nakala 10 za kitabu alichokuwa akikitumia kuhamasisha Waislamu
wasishiriki sensa iliyopangwa kuanza usiku wa kuamkia Agosti 26, mwaka
huu.
"Kukamatwa kwa mtu huyu kulitokana na taarifa zilizotolewa
na baadhi ya wananchi ambao miongoni mwao ni waumini wa Kiislamu ambao
walihisi kuchanganywa na taarifa hizo.
"Wakati Shekhe Koosa
akitoa taarifa yake, baadhi ya waumini walikubaliana naye lakini wengine
walimpinga hivyo ukatokea mtafaruku ndipo wale wenye dhamira ya
kushiriki sensa wakatoa taarifa polisi ambao walikwenda kumkamata,"
alisema.
Alisema baada ya kukamatwa, alipelekwa Kituo cha Polisi
Mombo kwa mahojiano na kudai kuwa, kile alichokuwa akikisema hakujua
kama kilikuwa na madhara pia ni kinyume cha sheria za nchi.
Aliongeza
kuwa, baada ya mahojiano Shekhe Koosa alihamishiwa Kituo cha Polisi
Wilaya ya Korogwe, kutokana na tishio la baadhi ya Waislamu kutaka
kuandamana ili kupinga kukamatwa kwake.
"Tunatarajia kumfikisha
Mahakamani wakati wowote baada ya taratibu za kuandaa mashtaka
kukamilika, naomba watu wengine wanaohamasisha wenzao kutoshiriki sensa
waache mara moja," alisema Kamanda Massawe.
No comments:
Post a Comment