SIKU chache baada ya Gazeti la MwanaHalisi kufungiwa kwa muda
usiojulikana, Serikali imepewa siku saba kuhakikisha inalifungulia bila
masharti yoyote kwa sababu ya kuandika habari zinazomuhusu Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari Dkt. Steven Ulimboka.
Mwenyekiti wa Kamati ndogo iliyoundwa baada ya
Serikali kulifungia gazeti hilo, Bw. Marcossy Albanie, aliyasema hayo
Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema
kama Serikali itashindwa kufanya hivyo, asasi mbalimbali za kiraia
zitaitisha maandamano makubwa nchi nzima kupinga hatua ya kufungiwa
gazeti hilo bila sababu za msingi.
Aliongeza kuwa, maandamano
hayo yataitishwa na wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu pamoja na
waandishi wa habari kwani sheria iliyotumika kulifungia gazeti hilo ni
kandamizi.
"Serikali imelituhumu gazeti hilo kwa kuchapisha
habari ambazo zinakiuka vifungu vya sheria ya magazeti namba tatu ya
mwaka 1976, habari iliyoandikwa inahusu kutekwa kwa Dkt.Ulimboka,
kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande,"alisema.
Bw.
Albanie alisema Serikali imetumia mabavu kulifungia gazeti hilo kwani
hawakutaka kusikiliza upande wa pili ambapo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo
Pinda, anafahamu sheria iliyotumika ni ya kikatili na imepitwa na
wakati.
"Serikali itekeleze haraka suala hili ndani ya siku
saba, asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Bw. Pinda ya kutaka
wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu sheria ya magazeti
hairuhusu ukataji rufaa kwa Waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na
kutoa hukumu,"alisema.
Aliongeza kuwa, Bw. Pinda hakusema kama
amepokea malalamiko ya gazeti hilo kuandika habari ya kichochezi hivyo
hiyo ni njia mojawapo ya kukwepa wajibu wake.
"Serikali
inashinikiza MwanaHalisi waende mahakamani wakati kesi nyingi
zinacheleweshwa zikiwa huko hivyo hali hiyo itasababisha gazeti hili
kutopata haki," alisema Bw. Albanie.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania
(MISA), Bw. Tumaini Mwailenge, aliitaka Serikali kulishughulikia tatizo
hilo haraka na kuondokana na sheria kandamizi kwa vyombo vya habari.
Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia suala la kufungiwa kwa Gazeti la
Mwanahalisi, Bw. Marcossy Albanie (katikati) akitoa tamko kwa waandishi
wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuitaka Serikali
ilifungulie gazeti hilo ndani ya siku 7. Kushoto ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania
(MISA-Tan), Bw. Mohammed Tibanyendera na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bw.
Tumaini Mwailenge
No comments:
Post a Comment